Friday, June 14, 2013

RONALDO AKANUSHA MPANGO WA KUONGEZA MKATABA REAL MADRIDCRISTIANO Ronaldo ametumia ukurasa wake wa Twitter kukanusha uvumi kwamba anajiandaa kusaini mkataba mpya na Real Madrid.

Ripoti nchini Hispania zilidai jana kwamba mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno anajiandaa kusaini mkataba mpya utakaomweka Bernabeu hadi mwaka 2018, huku pia rais wa klabu hiyo Florentino Perez akisisitiza kwamba mshambuliaji huyo anataka kubaki.

Hata hivyo, Ronaldo amesema madai hayo si kweli.

"Habari zote kuhusu mimi kusaini mkataba Real Madrid ni za uongo," alisema kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter.

Mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d'Or ya mwanasoka bora wa dunia 2008 amekuwa akihusishwa vikali na mipango ya kutimka Santiago Bernabeu katika wiki za karibuni, huku klabu inayotumia pesa nyingi kusajili wachezaji wapya ya Monaco ikisemekana kuandaa euro milioni 100 kwa ajili ya kumnasa.

Ronaldo, ambaye mkataba wake na Madrid unamalizika 2015, amekuwa akiripotiwa kwa muda mrefu kutokuwa na furaha Bernabeu, atajikuta akipata pesa nyingi zaidi ya anacholipwa sasa kama atahamia Monaco.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kurejea Manchester United, ingawa mabingwa hao wa Ligi kuu ya England hawataweza kufikia ofa ya mshahara wa euro milioni 20 kwa mwaka aliyoandaliwa na klabu iliyopanda daraja Ufaransa msimu huu ya Monaco.

----------------

No comments:

Post a Comment