Thursday, May 16, 2013

TANZANIA YAJITOA COSAFA


Tanzania (Taifa Stars) imejitoa kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayofanyika nchini Zambia kuanzia Julai 2-26 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah amesema Stars ambayo iliingizwa katika michuano hiyo kama timu mwalikwa imejitoa kutokana na mwingiliano wa ratiba kati ya michuano hiyo na mechi za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Amesema awali Tanzania ilithibitisha kushiriki michuano kwa matarajio kwamba Uganda ingekubali ombi la TFF la kubadilisha ratiba ya mechi za CHAN, lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) likagoma kwa vile kipindi ambacho kilipendekezwa lenyewe litakuwa na uchaguzi wa viongozi wao.

Taifa Stars itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi za CHAN ambapo mechi ya kwanza itachezwa jijini Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu wakati ya marudiano itafanyika jijini Kampala kati ya Julai 26-28 mwaka huu.

Akizungumzia michuano ya COSAFA, Kocha Kim amesema angependa kushiriki michuano hiyo kwani ingekuwa kipimo kizuri kwa kikosi chake, lakini kwa sasa malengo makubwa ya Stars kwenye mechi za mchujo za Kombe la Dunia na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo fainali zake zitafanyika mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment