Thursday, May 16, 2013

BECKHAM ASTAAFU SOKAMANCHESTER, England
MWANASOKA anayejulikana zaidi wa Uingereza, David Beckham ametangaza kustaafu soka leo baada ya maisha ya kimafanikio ya mchezo huo yaliyopambwa na kutwaa makombe mengi na umaarufu mkubwa duniani ulio zaidi ya soka.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 38, ambaye mwezi huu aliisaidia klabu ya PSG kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa na kuongeza katika idadi ya mataji aliyoyatwaa England, Hispania na Marekani, atatundika madaluga mwisho wa msimu huu.

"Nawashukuru PSG kwa kunipa fursa ya kuendelea lakini naona sasa ni wakati mwafaka wa kustaafu, nikicheza katika soka la daraja la juu," kiungo huyo alisema katika taarifa yake.

"Nataka kuwashukuru wachezaji wenzangu, makocha bora ambao nimenufaika kujifunza kutoka kwao. Napenda pia kuwashukuru mashabiki ambao wamekuwa wakinisapoti na  kunipa ungangari wa kufanikiwa."

Beckham aliichezea timu ya taifa ya England mechi 115, rekodi ambayo ni ya juu kwa mchezaji ambaye alikuwa bado akicheza, na alitwaa kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, mataji sita ya Ligi Kuu na Kombe la FA akiwa na Manchester United.

Alishinda mataji pia ya Ligi Kuu akiwa na Real Madrid nchini Hispania, LA Galaxy nchini Marekani na PSG nchini Ufaransa.

Mzaliwa huyo wa mji wa London, alianza maisha yake ya soka kwa kuichezea Manchester United, klabu ambayo aliishabikia tangu utotoni, na kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment