Sunday, April 7, 2013

BAYERN MUNICH YATWAA UBINGWA BUNDESLIGA... YAWEKA REKODI YA KULIBEBA TAJI MAPEMA ZAIDI

Wachezaji wa Bayern Munich wakishangilia ubingwa

BAYERN Munich walitwaa ubingwa wa Bundesliga zikiwa zimebaki mechi sita ligi kumalizika - na hivyo kuwa ni ubingwa uliotwaliwa mapema zaidi katika historia ya ligi kuu ya Ujerumani.

Bastian Schweinsteiger alifunga goli pekee la mechi hiyo ugenini dhidi ya Eintracht Frankfurt akimalizia kwa kisigino.

Bayern wamepoteza mechi moja tu msimu huu, wakiruhusu magoli 13 tu, na wameshinda mechi zao zote 11 tangu likizo ya Krisimasi.

Mabingwa watetezi Borussia Dortmund waliwafunga Augsburg 4-2 lakini wako pointi 20 nyuma.

"Ukweli kwamba tumetwaa taji hili baada ya mechi 28 ni jambo la kipekee, kwa ufupi ni babkubwa," alisema kocha Jupp Heynckes, ambaye anaachia madaraka mwisho wa msimu kumpisha Pep Guardiola kuifundisha timu hiyo.

"Moja ya mambo ambayo FC Bayern wameonyesha msimu huu ni kwamba sisi ni klabu kubwa, lakini tumethibitisha hilo kwa 'mizuka' kwenye timu."

Goli la Schweinsteiger lilikuwa wakati nahodha Philipp Lahm alipompigia krosi iliyomkuta kiungo huyo aliyemtungua kipa kiutamu kwa kisigino.

Kwa upande mwingine, ushindi wa Dortmund haukuwa na maana katika kubakisha kombe hilo ambalo walilitwaa kwa misimu miwili iliyopita.

Bayern sasa wanafukuzia kukamilisha kutwaa mataji matatu; la Bundesliga (ambalo washalibeba), Kombe la Ujerumani na la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya - jambo ambalo timu hiyo ya Ujerumani haijawahi kufanikiwa.

Hawajafungwa katika mechi za ugenini msimu huu hadi sasa, na kwa pointi 75 walizonazo kufikia sasa, wanaifukuzia rekodi ya kuzoa pointi nyingi katika msimu ambayo inashikiliwa na Dortmund ambao walipata pointi 81.

Baada kutwaa ubingwa wao wa 23, Bayern sasa wanaweka akili yao katika mataji mengine.

Wakiongoza kwa mabao 2-0 baada ya mechi yao ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Klabu BIngwa Ulaya dhidi ya Juventus, kikosi cha Heynckes kina nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele na wanaweza kukutana na mahasimu Dortmund, ambao walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Malaga.

Watawakabili Wolfsburg katika nusu fainali ya Kombe la Ujerumani, wakiwania kutwaa taji hilo la DFB-Pokal kwa mara ya 16.

Kocha wa Bayern, Jupp Heynckes ametwaa taji lake la tatu la Bundesliga - miaka 23 tangu alipotwaa la pili.

No comments:

Post a Comment