Xavi |
Messi |
Xavi Hernández hatacheza mechi ya kesho Jumamosi (Machi 2, 2013) ya 'el clasico' kati ya Barcelona na Real Madrid katika marudiano yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Kiungo huyo anasumbuliwa na jeraha la paja, na kipaumbele cha Barca sasa ni kuona kuwa anakuwa 'fiti' kucheza Jumanne (Machi 12) mechi yao ya marudiano ya hatua ya 16-bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Milan kwenye Uwanja wa Camp Nou. Barca walishachapwa 2-0 katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Milan iliyochezwa kwenye Uwanja wa San Siro. Wanaongoza La Liga kwa tofauti ya pointi 12 dhidi ya Atletico Madrid wanaowafuatia katika nafasi ya pili na 16 dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Real Madrid wanaoshika nafasi ya tatu.
Xavi tayar alishajitoa mhanga Jumanne kwa kucheza katika mechi ya 'Clásico' dhidi ya Real Madrid iliyokuwa ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme ingawa alikuwa hayuko 'fiti' na alionekana wazi kucheza chini ya kiwango huku wakichapwa 3-1 kwenye uwanja wao wa Camp Nou.
Wakati Xavi alipocheza dhidi ya Valencia February 2, alilazimikakutoka uwanjani huku akiwa na maumivu mguuni.
Jeraha dogo lilionekana, lisilofikia ukubwa wa sentimita. Iliamuliwa kwamba ni lazima apumzike ili awe fiti kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Milan kwenye Uwanja wa San Siro. Na hivyo ndivyo alivyopata nafasi ya kucheza akiwa mzima mjini Milan.
Alicheza pia dhidi ya Sevilla. Hakuwamo katika kikosi kilichoanza lakini akaingia katika dakika ya 22 kabla ya kutolewa kuelekea mwishoni mwa mechi na nafasi yake kutwaliwa na Iniesta.
Tatizo kubwa zaidi likaibuka mazoezini katika siku iliyofuata. Wakati akiendelea kujifua vikali na wenzake, kiungo huyo akajitonsha katika jeraha lilelile la kwanza.
Xavi hatakuwamo katika kikosi kitakachocheza dhidi ya Real Madrid na baada ya hapo atakuwa na wiki nzima ya kujiweka tena fiti kwani Barça hawatakuwa na mechi Jumanne wala Jumatano.
Xavi ndiye anayeongoza miongoni mwa wachezaji wa kizazi cha sasa kucheza 'Clasico' nyingi baada ya kuwamo katika mechi 37. Vinara wa mechi nyingi za Clasico ni Manolo Sanchis aliyecheza mechi 43 na Francisco Gento aliyechez Clasico 42.
MESSI ABANWA HOMA, FLU
Lionel Messi amekosa mazoezi ya leo asubuhi baada ya kusumbuliwa na maradhi ya homa na flu, kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya klabu yake ya Barca.
Jana (Alhamisi Februari 28, 2013), wachezaji waliruhusiwa kupumzika na hata hivyo, Barça wanaamini kwamba atapata nafuu na kucheza mechi yao ya kesho ya marudiano ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
No comments:
Post a Comment