Wednesday, March 13, 2013

SIMON MSUVA KUTOKA KUDANSI THT HADI KUWAKIMBIZA MABEKI KATIKA SOKA

 Na www.sufianimafoto.com
KAMA hujawahi kupata fursa ya kumuona na unasikia tu jina na mambo afanyao uwanjani, huwezi kudhani kama anayetajwa ni mtu mwenye mwili usioendana na mambo makubwa afanyayo ndani ya dimba. 

Ni kijana mdogo, mwembamba, mfupi, mwenye sura yenye haiba ya aibu wakati mwingi na asiye na maneno mengi ya kuzungumza katika kadamnasi lakini nyuma yake kuna vitu vingi vilivyojificha.

Huyu ni winga machachari na mwenye kasi wa Dar Young Africans, Simon Msuva, ambaye amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Moro United ambayo sasa ipo Ligi Daraja la Kwanza baada ya kushika daraja msimu uliopita ambako pia ina hali mbaya.

Msuva anayefanana kiuchezaji na Mrisho Ngassa, anasifika kwa uwezo wa kupiga chenga, kukimbia na mpira na kupiga krosi kali zenye madhara kwa timu pinzani japokuwa kuna wakati hujisahau na kutaka kufunga mwenyewe hata akiwa eneo gumu kufanya hivyo.

KUTOKA DANSA HADI SOKA:-

Msuva kama ilivyo kwa vijana wengine wanaoweza kujaribu maisha kupitia fani mbalimbali, mwaka 2004 hadi 2005, alikuwa akishiriki kucheza muziki katika kundi la Tanzania House of Talent (THT) akiwa kama mwanafunzi wa 'kudansi'.

Lengo la Msuva lilikuwa kutazama labda angeweza kufikia mafanikio ya maisha yake kupitia muziki na siyo kwa kuimba wala kutunga nyimbo, bali kucheza muziki na hii ni kutokana na kupenda zaidi muziki na kuwa na marafiki wengi walio wanamuziki na zaidi wale wa kudansi.

“Nilidhani kazi ya kucheza muziki ingeweza kunisaidia kunitoa na kufikia malengo yangu, lakini mambo hayakuwa hivyo kwani baada ya muda mfupi tu nikiwa najaribu kushiriki na rafiki zangu wa THT, nikaona kucheza muziki kunaweza kunichukulia muda mwingi kabla ya kupata mafanikio katika maisha,” anasema Msuva.

Baadhi ya vijana ambao Msuva alikuwa akicheza nao muziki THT ni Msami na Malenga ambao anadai walikuwa rafiki zake wa damu wakiwa katika kundi hilo na wote walikuwa na malengo ya kufika mbali kupitia muziki.

AJIKITA UWANJANI:-
Kutokana na kuwa Vipaji viwili na vyote akiamini kuvimudu vilivyo, Mwaka 2006, Msuva alijiunga na timu ya mchangani inayojihusisha na ukuzaji wa vipaji vya vijana wadogo ijulikanayo kwa jina la Wakati Ujao, ambayo aliichezea hadi mwaka 2007 alipojiunga na timu ya Academy.

 Akicheza kama mshambuliaji wa kati na wakati mwingine winga, Msuva aliichezea Academy hadi mwaka 2008, alipojiunga na timu ya kukuza vipaji vya vijana ya Azam ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa.

Ndoto zake za kucheza soka nusura zifikie ukingoni baada ya timu hiyo ya Azam kuvunjika mwaka 2008 mwishoni, jambo lililomfanya Msuva kurejea katika kituo cha Academy kuendelea kujifunza soka.

ANG’ARA COPA COCA COLA:-

Akizungumza na mtandao huu wa www.sufianimafoto.com, baada ya kufanya vizuri akiwa na kikosi cha Academy, mwaka 2009 na 2010, Msuva alichaguliwa kucheza michuano ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ya Copa Coca Cola, na kupata nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17.

Akiwa na timu hiyo ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys, Msuva alijiunga na vijana wenzake kuelekea katika mechi ya timu hiyo iliyochezwa Sudan.

ATUA MORO UNITED:-
Baada tu ya kurejea nchini Uwezo, juhudi na kufuata vyema maelekezo ya mwalimu na kuweza kuwika dimbani kwa Msuva akiwa na Serengeti Boys, kulimfanya kinda huyo kuonekana na kuvutiwa na Klabu ya Moro United, waliomsajili katika kikosi chao cha vijana mwaka 2010.

Akiwa Moro United, Msuva alifanya vizuri kiasi cha kuibuka mfungaji bora wa michuano ya vijana wa timu za Ligi Kuu ya Bara maarufu kama Uhai Cup, inayofanyika kila mwaka kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Baada ya kuibuka mfungaji bora katika Kombe la Uhai, Msuva alipandishwa hadi kikosi cha kwanza cha Moro United japokuwa hakuwa akipata nafasi mara kwa mara.

ARUDI AZAM:-
Akiendelea kufanya vizuri akiwa dimbani, Mwaka 2011, Msuva alihama Moro United na kuerejea Azam ambako alipelekwa kikosi B huku akiwa na nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Bara. Hata hivyo, pamoja na kurejeshwa katika kikosi cha Azam, Msuva anakiri kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa vijana wa akiba, mpango wa baadaye wa timu hiyo hivyo hakuweza kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza.

“Azam walinisajili hadi katika ligi kuu, lakini hawakuweza kunichezesha mechi za ligi kwa kuwa mimi nilikuwa mmoja wa wachezaji waliopanga kuwatumia siku za baadaye baada ya kupata uzoefu zaidi.

“Lengo lao lilikuwa mimi nianze kucheza kuanzia labda mwaka 2014, kwa kuwa umri wangu uliruhusu kuweza kusubiri huku nikiendelea kupata uzoefu kutoka kwa wachezaji wengine wa timu kubwa,” anasema Msuva.

Mwaka jana Msuva alirejea tena Moro United kabla ya kusajiliwa na Yanga mwaka huohuo.

ANAPENDA KUCHEZA NA TEGETE, ANAMKUBALI BARNABA THT:-
Huku akisuasua, Msuva anasema anapenda zaidi kucheza sambamba na mshambuliaji Jerry Tegete, japokuwa anapenda kucheza na washambuliaji wote wa Yanga katika kikosi cha kwanza, sababu kubwa ikiwa ni ujanja wa Tegete awapo katika lango la timu pinzani.

“Washambuliaji wa Yanga wote naona ni wazuri kucheza nao, lakini Tegete ni mjanja zaidi mnapokuwa mnashambulia kwa kuwa ana uwezo wa kucheza mipira inayodharauliwa na adui zetun na pia kucheza mahala ambapo huamini kuwa angeweza kucheza.

“Unaweza kupiga mpira ukadhani (Tegete) hayupo eneo hilo, lakini ghafla unaweza kumuona ameshafika na kuucheza mpira, japoa hana speed kali lakini ni mjanja wa kujipozisheni tu. Pia ni mfungaji mzuri wa mabao ya vichwa,” anasema Msuva.
Kwa upande wa muziki, Msuva anamkubali zaidi Elius Barnaba ambaye naye ni zao la THT kama alivyo yeye. Anapenda jinsi anavyojituma kimuziki kutunga, kuimba na namna anavyoweza kuwasaidia wenzake.

“Namkubali sana Barnaba maana anajituma ipasavyo katika muziki wake na kazi zake nyingi ni nzuri na za kupendeza, yeye ni mfano mzuri kwa vijana wote ambao tunatafuta maisha kupitia sanaa na utamaduni,” anasema Msuva.

HAJAWASAHAU WASHKAJI ZAKE THT:-
Tofauti na mastaa wengine ambao husahau mahali walipotokea, Msuva mara kadhaa amekuwa akiwatembelea rafiki zake wa THT ambao alishirikiana nao katika kucheza muziki na hupiga nao stori kama kawaida.

“Siwezi kusahau nilipotoka, mara nyingi huwa naenda THT na kuzungumza mambo mbalimbali na rafiki zangu ambao wamebaki pale. Hakika ni kitu ninachojivunia siku hadi siku na naamini wao ni sehemu ya mafanikio yangu katika soka,” anasema Msuva.

Msuva anasema, akiwa THT hukutana na kuzungumza na wasanii wote hata wale ambao sasa hawapo kama Barnaba ambaye anakubali kazi zake na kupeana changamoto mbalimbali za kimaisha.

HAPENDI MARAFIKI WANASOKA:-

Unaweza kumuona ni mtu wa ajabu lakini ndivyo ilivyo hata kwa wanasoka wakubwa duniani, Msuva hapendi kujenga urafiki mkubwa na wachezaji wenzake kwa kuwa muda mwingi atakuwa akifikiria zaidi soka pekee na kupoteza mambo mengine katika jamii.

“Niliwahi kushauriwa na 'Kaka yangu' Mtemi Ramadhan, aliniambia kuwa kitu kimoja kikubwa sana katika maisha ya soka, ni kwamba sipaswi kuwa na marafiki wengi ambao ni wanasoka pekee ambao muda mwingi huzungumza lugha moja ya soka tu.

“Kama binadamu, napaswa kuwa na marafiki wanaojishughulisha na mambo mengine ili tu niweze kupanua wigo wangu wa uelewa na mawazo. Nadhani ni ushauri mzuri na naona unanijenga siku hadi siku na kunisaidia,” anasema Msuva.

CHANGAMOTO ZA YANGA, NAFASI KIKOSI CHA KWANZA:-
“Mimi bado ni kijana mdogo, Yanga ni timu kubwa na pia kuwa wachezaji wenzangu wengu tu wakubwa na wazoefu kunizidi, sasa kuna vitu lazima ukumbane navyo unapojiunga na timu kubwa kama hii lakini nashukuru Mungu nimeweza kujiunga na timu kubwa kama hii na kucheza kikosi cha kwanza,” anasema Msuva.

Anasema wachezaji wakongwe na wale wa kimataifa wanaendelea kuwa kioo kwake kwa maisha ya ndani na nje ya uwanja na mara kadhaa huwauliza kuhusu mambo mbalimbali ya soka.

“Mwanzo nilikuwa siamini kama nipo Yanga na wala nilikuwa siamini kuwa nacheza na wachezaji maarufu, lakini sasa nipo nao na naishi nao vizuri na wao ni washauri wazuri kwangu na naamini hadi kufikia hapa nilipo wao wameshiriki kwa kiasi kikubwa sana kunisaidia kwa namna moja ama nyingine,” anasema Msuva.

Mara nyingi Msuva hupokea ushauri kutoka kwa kiungo Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza, Athuman Idd Chuji na wakongwe wengine wa Yanga.

SASA SI KAZI BURE:-

Mwanzo wakati anaanza kupata nafasi kikosi cha kwanza cha Yanga, Msuva alikuwa anachezeshwa kama winga nafasi anayoicheza hadi leo hii, lakini mara nyingi alikuwa akikimbia na mpira muda mrefu huku akijaribuku kutaka kufunga hata kama yupo ‘impossible angle’, lakini siku hizi kwa kiasi kikubwa amebadilika, ambapo amekuwa akipiga krosi nyingi na zenye malengo.

“Unajua mimi wakati nasajiliwa Yanga kutoka Moro United, kule nilipotoka nilikuwa nacheza kama mshambuliaji sasa Yanga nachezeshwa kama winga hali inayonifanya niwe natamani zaidi kufunga kila ninapojisahau kuhusu nafasi niichezayo.

“Lakini kwa sasa namshukuru kocha ananielewa na sasa namimi nimemuelewa baada ya kuniambia nisiwe mchoyo wa pasi, niwe nawapa wenzangu pasi mapema na wala siharibu kama ilivyokuwa mwanzo. Nadhani sasa nacheza vizuri tofauti na mwanzo,” anasema Msuva.

ANAVUTIWA NA RONALDO, DOMAYO LAKINI ANAIPENDA MAN UTD:-
Ronaldo
Msuva ni shabiki mkubwa wa mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo na kiungo wa Yanga, Frank Domayo. Anasema anampenda Ronaldo, kutokana na aina ya uchezaji wake lakini Domayo ni zaidi ya mchezaji na rafiki kwake.

Frank Domayo (kulia)
“Domayo ni rafiki yangu katika kikosi cha Yanga pia navutiwa na aina yake ya uchezaji na pia huwa ananishauri mambo mbalimbali na hata mimi hufanya hivyo kwake. Ni mchezaji ambaye naamini atafika mbali katika soka la Tanzania,” anasema Msuva.
Wakati akionyesha wazi mapenzi yake kwa Ronaldo, Msuva ni shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United ya England na hilo haoni haya kulificha na yupo kifua mbele kuitetea klabu hiyo yenye maskani yake katika jiji la Manchester.

“Naipenda Man United, ni timu nzuri yenye kila kitu cha kuiwezesha kutwaa mataji mbalimbali ndani na nje ya England japokuwa tayari imeshatolewa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya,” anasema Msuva.

PIA NI KIONGOZI WA MITINDO YA KUSHANGILIA KATIKA KIKOSI CHA YANGA:-
Simon Msuva (katikati) akiongoza wenzake kuwashangili kwa kunyoosha kidole.

Tazama mechi yeyote ya Yanga kwa umakini, mara tu timu hiyo inapopata bao wachezaji wote humwangalia Msuva na kumfuata huku wakimfuatisha kucheza na yeye ndiye mbunifu wa mitindo yote ya uchezaji na hii inawezekana ni kutokana na yeye kuwa mkali wa kudansi hapoa awali.


“Tangu nilipokuwa Moro United, nilikuwa kinara wa kubuni mitindo ya kushangilia. Hapo naweza kubadilisha kutoka mmoja hadi mwingine kulingana tu na mechi yenyewe. Wachezaji wenzangu kabla ya mechi hunifuata na kuniuliza jinsi ya kushangilia mimi huwaelekeza nini cha kufanya,” anasema Msuva ambaye hana mke wala mtoto.

KWA TAARIFA YAKO…

Msuva aliyezaliwa mwaka 1993, na kusoma shule ya msingi ya Lions iliyopo Magomeni, Kinondoni jijini Dar es Salaam anapenda kuigiza sauti za wanamuziki kama Ben Pol na Belle Nine wanaoimba muziki wa kizazi kipya na pia hupenda sana kusikiliza nyimbo za wasanii hao.

Chipukizi huyu anapenda kunyoa nywele zake kwa mtindo wa kiduku, lakini hivi karibuni uongozi wa Yanga ulimpiga mkwara na kumshauri kuondoa staili hiyo ama kunyoa kabisa ili asiweze kuvimba kichwa.

“Nimeambiwa ninyoe nywele zangu, sina tatizo nimezinyoa lakini naamini mimi ni mkubwa na naweza kujiongoza katika mambo mbalimbali bila ya kupotea kama uongozi unavyodhani,” anasema Msuva ambaye bado anaishi na wazazi wake, huko maeneo ya Kimara jijini Dar.

MAKALA HII IMEANDALIWA NA MTANDAO WA www.sufianimafoto.com

No comments:

Post a Comment