Thursday, March 21, 2013

LWAKATARE WA CHADEMA ALIVYOACHIWA HURU NA KUKAMATWA TENA SEKUNDE CHACHE TU BAADAYE... ILIKUWA KAMA MCHEZO WA KUIGIZA KWENYE VIUNGA VYA MAHAKAKA YA KISUTU... APIGWA PINGU NA KUTUPWA LUPANGO KABLA YA KUSOMEWA MASHTAKA MENGINE YAKIWAMO YA KUPANGA NJAMA ZA KUMTEKA NYARA MHARIRI MTENDAJI WA GAZETI LA MWANANCHI ...!

Peopleeeeeeeeeees....! Lwakatare (kushoto)

Lwakatare (kushoto)
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana ilimwachia huru Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, na mwenzake baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya kuwafutia mashtaka washtakiwa hao.

Hata hivyo, baada ya washtakiwa hao kuachiwa huru chini ya kifungu namba 91 (1) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (ACP), walikamatwa na kufungwa pingu na askari polisi na kuwekwa chini ya ulinzi katika chumba cha mahabusu ya mahakama hiyo saa 3:30 asubuhi.

Uamuzi wa kuwaachia huru ulitolewa jana saa 3:00 asubuhi na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha hati ya kuwaondolea mashitaka washtakiwa hao kutoka kwa DPP.

Mawakili wa Serikali Wakuu, Prudence Rweyongeza, Ponsiano Lukosi wakisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Mauggo, waliwasilisha hati hiyo kwamba DPP hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao na kwamba amewaondolea mashtaka hayo.

“Kesi hii ilipangwa kusikilizwa uamuzi wa hoja zilizotolewa na mawakili wa pande zote mbili, lakini kutokana na DPP kupitia upande wa Jamhuri kuwasilisha hati ya kuwaondolea washtakiwa mashtaka, mahakama hii inawaachia huru,” alisema Hakimu Mchauru.

Hata hivyo, baada ya kutoka kwenye ukumbi namba moja wa mahakama, washtakiwa hao walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Ilipofika saa 4:45 asubuhi, washtakiwa walipandishwa kizimbani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi huku wafuasi wa Chadema wakiwa wamefurika katika viunga vya mahakama hiyo na kusimama kwenye makundi makundi.

Rweyongeza aliomba mahakama kuwasomea washtakiwa hao hati mpya ya mashtaka, na kudai kuwa wanakabiliwa na mashtaka manne ikiwamo kula njama ya kutaka kutoa sumu, kufanya mkutano wa ugaidi na kupanga tukio la kumteka nyara Dennis Msacky.

Lwakatare na mwenzake Ludovick Rwazula walifikishwa katika viunga vya mahakama hiyo jana saa 2:00 asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi.

Wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, baadhi ya wabunge wa chama hicho na wanafamilia ya Lwakatare waliingia katika eneo la mahakama kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

 Washtakiwa hao walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aloyce Katemana.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Prudence Rweyongeza, Ponsiano Lukosi wakisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Mauggo.
 Wakili Rweyongeza akiwasomea washtakiwa hao mashtaka hayo, alidai kuwa Desemba 28, mwaka 2012 katika eneo la King’ongo, Kimara Stopover jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikuwa njama ya kutenda kosa la jinai kwa nia ya kumdhuru Dennis Msacky kwa kumpa sumu.

 Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Kifungu cha 227.

 Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza, washtakiwa hao walishirikiana kula njama ya kumteka nyara Msacky kinyume cha kifungu cha 4 (2) (c) cha Sheria ya Ugaidi.

Rweyongeza aliendelea kusoma shtaka la tatu katika ukumbi namba moja wa mahakama hiyo uliokuwa umefurika mamia ya watu wakiwamo wafuasi wa Chadema kuwa, Desemba 28, mwaka 2012 katika eneo la King’ongo, Kimara  Stopover, jijini Dar es Salaam, washtakiwa Lwakatare na Rwazula walipanga kushiriki mkutano wa kumteka nyara Msacky.

Katika shtaka la nne, upande wa mashtaka ulidai kuwa, siku na eneo la tukio la tatu, mshtakiwa wa kwanza Lwakatare, akiwa mwenye nyumba aliruhusu kufanyika mkutano wa kupanga tukio la utekaji nyara kwenye nyumba yake huku akijua ni kosa kwa mujibu wa sheria ya ugaidi.

Jumatatu iliyopita, washtakiwa hao walihojiwa na mahakama kama tuhuma hizo ni za  kweli au siyo kweli na wote walizikana.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mashtaka ya ugaidi yanayowakabili washtakiwa, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa chombo chenye mamlaka hayo ni Mahakama Kuu, hivyo hawakutakiwa kujibu chochote na walipelekwa rumande.

Kutokana na hali hiyo, baada ya upelelezi kukamilika kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Upande wa utetezi uliongozwa na mawakili Profesa Abdallah Safari na Peter Kibatala ambao waliomba mahakama kuwasilisha hoja zao, lakini Hakimu Katemana alisema kama kutakuwa na masuala yoyote ya kuwasilishwa mahakamani hapo yatafanyika Aprili 3, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.

No comments:

Post a Comment