Thursday, January 31, 2013

SARE DHIDI YA READING YAMCHANGANYA BENITEZ

Frank Lampard wa Chelsea akishangilia goli lake wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Reading kwenye Uwanja wa Madejski mjini Reading, England jana Januari 30, 2013. Timu hizo zilitoka 2-2.

KOCHA wa Chelsea, Rafael Benitez amesema ameachwa akiwa amechanganyikiwa baada ya timu yake kushindwa kuifunga timu inayopigania kutoshuka daraja ya Reading kwenye Uwanja wa Madejski jana usiku.

Chelsea walipoteza uongozi wao wa magoli 2-0 wakati mchezaji wa akiba Adam Le Fondre alipofunga mara mbili na kulazimisha sare ya 2-2 ya dakika za lala salama.

"Ni ngumu kuelezea ni vipi tumetoka sare mechi hii," alisema Benitez.

"Tulifanya kila kitu ili kushinda mechi hii. Kwa dakika 85 tulitawala kila kitu na kutengeneza nafasi za kutosha kufunga magoli manne ama matano. Ni ngumu kuikubali."

Chelsea iliyo katika nafasi ya tatu ilionekana kama inaelekea kushinda mechi yake ya tano mfululizo ya ugenini kufuatia magoli kutoka kwa Juan Mata na Frank Lampard kufunga magoli ya kuongoza.

Lakini walishangazwa mara mbili katika dakika za lala salama wakati Reading walipopata pointi ambayo imewasaidia kutoka kuwenye ukanda wa kushuka daraja.

No comments:

Post a Comment