Monday, January 14, 2013

MABAO 10 AMBAYO MWAIKIMBA HATAYASAHAU


Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
AZAM juzi ilitetea Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-1 ndani ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao lao la ushindi likifungwa na Gaudence Exavery Mwaikimba. Je, wajua mabao 10 ambayo amefunga mshambuliaji huyo na hatayasahau daima maishani mwake? Endelea.

10. Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2013 kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, wakati Gaudence alipopokea pasi ya Brian Umony na kuwahadaa mabeki wa Tusker FC ya Kenya, kabla ya kufumua shuti kali lililotinga nyavuni. Anasema hatalisahau bao hili kwa sababu liliipa timu yake, Azam FC Kombe la Mapinduzi naye akitoka uwanjani kama shujaa wa mchezo.

9. Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2005, akichezea timu ya mkoa wa Mbeya, wakati alipowazidi nguvu na maarifa mabeki wa Mtwara kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuifungia Mbeya bao la pili na la ushindi ndani ya dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1. Anasema hatalisahau bao hili, kwa sababu liliipa Kombe Mbeya na kumjengea yeye heshima nyumbani, kama mmoja wa wanasoka wakubwa waliowahi kutokea Mbeya.

8. Ilikuwa ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2011 dhidi ya Mwanza, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha alipoifungia Mbeya bao pekee la ushindi dakika za majeruhi baada ya kutimu dakika 90 za kawaida za mchezo. Anasema hawezi kulisahau bao hilo, kwa sababu lilimuwezesha pia kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kuzidi kujijengea heshima Mbeya.

7. Ilikuwa ni katika Ligi Kuu ya Bara mwaka 2005 akiichezea Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam alipoinusuru kuzama mbele ya Yanga kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha baada ya kuifungia bao la kusawazisha na kuwakatili Watoto wa Jangwani kuondoka na pointi tatu. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu ni kama lilimfungulia njia ya kusajiliwa Yanga, kwani tangu siku hiyo ndipo viongozi wa timu hiyo walipoanza kuzungumza naye, hatimaye wakamsajili 2006.

6. Ilikuwa ni mwaka 2007 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kati ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo alipoifungia bao Stars lililoelekea kuwa la ushindi dhidi ya Angola Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kabla ya mshambuliaji wa zamani wa Manchester United ya England, Manucho kuisawazishia Angola. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu lilimjengea heshima katika medani ya kimataifa, kwa sababu Angola wakati huo ilikuwa imetoka kucheza Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.

5. Ilikuwa ni mwaka 2006 kwenye michuano ya Kombe la Tusker, wakati Gaudence Mwaikimba alipovunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Moro United na kumtungua kipa Amani Simba, kuifungia Yanga bao la pili akitoka kufunga pia la kwanza. Anasema analikumbuka bao la pili kwa sababu, baada ya kufunga Moro United waligomea mechi na mchezo ukaishia hapo, Yanga ikitinga Nusu Fainali.

4. Ilikuwa ni mwaka 2012 katika siku zake za mwanzoni kabisa Azam, wakati alipoifungia timu hiyo bao la ushindi kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba SC Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika dakika za mwishoni kabisa za mchezo wakishinda 2-1. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu liliipeleka Azam fainali ya michuano hiyo, ambako walifanikiwa kutwaa Kombe la kwanza katika historia ya timu hiyo.

3. Ilikuwa ni mwaka 2006 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Rwanda wakati Gaudence Mwaikimba alipofunga bao pekee la ushindi timu ikiwa chini ya kocha Dk. Mshindo Msolla. Anasema hawezi kulisahau bao hilo kwa sababu siku hiyo ndiyo kocha Mbrazil, Marcio Maximo alikuwa amewasili nchini na alikuwa jukwaani akiangalia wachezaji, hivyo kufanya kwake vizuri kulimfanya aendelee kuwa timu ya taifa chini ya kocha huyo wa Kibrazil.

2. Ilikuwa ni mwaka 2007 katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame wakati Mwaikimba alipoifungia Yanga bao la kwanza kati ya mawili ya kusawazisha, la pili likifungwa na Mkenya Ben Mwalala hivyo kufanya sare ya 2-2. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu liliirudisha timu yao mchezoni ikitoka nyuma kwa 2-0 na kupata sare ya 2-2 hivyo kuingia Robo Fainali ya michuano hiyo mjini Kigali, Rwanda.  

1.ilikuwa ni mwaka 2006 katika msimu wake wa kwanza kwenye klabu ya Yanga, Mwaikimba alipoifungia Yanga bao la tatu, baada ya kufunga mawili ya awali pia katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Anasema hatalisahau bao hilo kwa sababu lilikamilisha hat-trick yake pekee katika Ligi Kuu kihistoria hadi sasa na kufanya mashabiki warejee makwao siku hiyo wakiimba jina lake.

Naam, hayo ndio mabao 10 ambayo Gauedence anasema ataendelea kuyakumbuka daima kati ya mabao aliyowahi kufunga.

Mwaikimba, akishangilia moja ya mabao aliyofunga 
WASIFU WAKE:
JINA: Gaudence Exavery Mwaikimba
KUZALIWA: Oktoba 5, 1984
ALIPOZALIWA: Kyela, Mbeya
KLABU YAKE: Azam FC
KUJIUNGA: 2012
KLABU ZA AWALI:
Mwaka               Klabu 
2003-2004:        Tukuyu Stars
2004- 2005:       Kahama United
2005- 2006:       Ashanti United
2006- 2009:       Yanga SC
2009-2010:        Sur (Oman)
2010:                   Prisons FC
2011- 2012:       Kagera Sugar
2012:                   Moro United
2012 hadi sasa   Azam FC
Mwaikimba akifurahia na mashabiki wake Kombe la Mapinduzi jana

No comments:

Post a Comment