Wednesday, December 5, 2012

SERIKALI YALITAKA SHIRIKA LA KAZI DUNIANI KUUTUNISHA MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani, Bibi Hopran Fololo wakati akimwelezea kuhusu utekelezaji wa mpango wa Ujasiriamali kwa Vijana unaoendeshwa na Shirika hilo hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Dkt. Elisante Ole Gabrieln na wengine ni wajumbe  kutoka ILO.
(Picha na Concilia Niyibitanga, WHVUM)

Na Concilia Niyibitanga, WHVUM
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imelitaka Shirika la Kazi  Duniani (ILO) kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili vijana wengi waweze kukopa na kuanzisha miradi ya ujasiriamali.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na ujumbe kutoka Shirika hilo uliokuja ofisini kwake kwa ajili ya kuzungumzia Mradi wa Ujasiriamali kwa vijana unaoendeshwa na Shirika hilo.

Dkt. Mukangara pia amelitaka ILO kupitia mradi huo kutoa mafunzo husika katika vituo vya Vijana vya Sasanda, Marangu na Ilonga kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa vituo hivyo.

Akielezea mpango huo, Mkurugenzi Msaidizi Mkaazi wa Shirika hilo, Bibi Hopran Fololo amesema kuwa wataanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 225 waliomaliza Vyuo Vikuu katika fani mbalimbali na baadae vijana hao watatakiwa kwenda vijijini kuhamasisha vijana wenzao kuhusu elimu ya ujasiriamali na umuhimu wake.

Bibi Fololo amesema kuwa Shirika kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wanatarajia kuingiza elimu ya Ujasiriamali katika mitaala ya elimu ya Sekondari na Vyuo vya Ualimu kwa lengo la kuwawezesha vijana kuhitimu wakiwa na elimu hiyo jambo amabalo litawasaidia kujiajiri wenyewe.

Katika mradi huo wenye lengo la kuibua fursa za ajira kwa vijana kupitia ujasiriamali shirika litatoa mafunzo kwa Maafisa Vijana wa Wilaya nchi nzima ili waweze kuwaongoza vijana ipasavyo katika sekta ya ujasiriamali. Ameongeza Bibi Fololo.

Aidha, Fololo amesema kuwa Shirika litatoa ruzuku kwa baadhi ya miradi itakayobuniwa na vikundi vya vijana ambapo vikundi vitashindanishwa na washindi kupatiwa ruzuku ya kuanzia Dola 15,000 hadi Dola 20,000 kwa ajili ya kuendesha miradi yao.

Ameendelea kueleza kuwa pamoja na kutoa ruzuku kwa vikundi vya vijana, watazisaidia pia taasisi za fedha zinazokopesha vijana kwa kuzitunishia mifuko ili ziwe na uwezo wa kukopesha vijana wengi zaidi.

Mradi huu unalenga kuhamasisha vijana wapatao milioni moja na nusu katika maswala ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wenyewe.

No comments:

Post a Comment