Tuesday, December 25, 2012

EL SHAARAWY: KIJANA MDOGO WA MISRI ANAYEBEBESHWA ZIGO KUBWA LA MILAN


*Badala ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji baada ya kumpoteza Ibrahimovic, Milan inaegemea mno mabega madogo ya El Shaarawy.

Stephan El Shaarawy
Stephan El Shaarawy


MIEZI sita iliyopita Zlatan Ibrahimovic alikuwa mchezaji muhimu Milan na maoni pekee yaliyotolewa na mtu yeyote kuhusu Stephan El Shaarawy yalizungumzia nywele zake tu.

Rino Gattuso alilalamikia tabia ya El Shaarawy ya kunyoa nyusi zake. Wachezaji wenzake kadhaa walitishia kumnyoa nywele zake za upanga wa jogoo, zilizopewa jina la "La Cresta" nchini Italia.

"Natumai atafunga angalau magoli 15," nahodha Massimo Ambrosini alisema Juni mwaka huu. "Kama hatafanya hivyo, nitamkata 'kiduku' chake. Kama atafunga saba kabla ya Krismasi, nitamlipia gharama za sikukuu yake."

El Shaarawy alitimiza hilo tangu Oktoba. Ambrosini aliongeza ofa ya kumpeleka mapumzikoni kwenye milima ya Caribbean kama Farao Mdogo huyo (baba yake ni Mmisri) atafunga magoli 10.

Kijana huyo pia ametimiza hilo ambapo hivi sasa anaongoza orodha ya wafungaji wa Serie A akiwa na magoli 14, moja juu ya Edinson Cavani; wakati Miroslav Klose na Antonio Di Natale wana magoli 10. Ambrosini, hakutaka kuongeza ofa.

Hivi sasa, wakati El Shaarawy akipaa kwenda mapumziko (ripoti zinadai ameishia kwenda Dubai), ameibuka kuwa mtu muhimu Milan kama alivyokuwa Ibrahimovic.

Mwaka jana, Milan ilifunga jumla ya magoli 80 katika Serie A na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya. Ibrahimovic alihusika katika magoli 43 kati ya hayo (alifunga 28 na kupika sita katika ligi, na alifunga matano na kupika manne Ulaya). Msimu huu, El Shaarawy amefunga ama kupika magoli 17, nusu ya magoli 34 waliyofunga Milan kwenye ligi.

"El Shaarawy anacheza vyema zaidi ya tulivyomtarajia," Adriano Galliani alisema. "Ndiyo kwanza ametimiza umri wa miaka 20 wiki iliyopita na sijui ni washambuliaji wangapi wa umri wake wanaofunga mfululizo kama yeye. Mchezaji mwingine kama yeye duniani ni Neymar."

Kama Neymar, El Shaarawy anaingia ndani ya boksi kutokea upande wa kushoto ili apige kwa mguu wake wa kulia. Lakini yuko vizuri kwenye upande wa kushoto pia. Arsene Wenger, Cesare Prandelli na Paolo Maldini wote wamesifu mchango wake katika kusaidia ulinzi pia. Gattuso "amemvulia kofia" na kukiri kwamba hakuwa sahihi kumpuuza mchezaji mwenzake. Andriy Shevchenko anaona njia ya mafanikio yake kama anayokuja nayo El Shaarawy.

Mshambuliaji huyo ameinukia haraka. Wiki chache baada ya sherehe yake ya kutimiza umri wa miaka 16 aliweka rekodi ya mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kupata kuichezea timu ya wakubwa katika ligi kuu ya Italia wakati alipoichezea Genoa kwa mra ya kwanza. Alikwenda kwa mkopo Padova mwaka uliofuata na akaisaidia timu hiyo kufikia hatua ya "kapu" ya kuwania kupanda Serie A. Alishinda tuzo ya mwanasoka kijana ligi daraja la pili Italia na Milan wakanunua nusu ya haki zake.

"Alipowasili hapa akitokea Padova alikuwa na matatizo mengi ya kutokuwa fiti, lakini yuko vyema sasa na ni mmoja wa vipaji vikubwa zaidi vya soka duniani," Galliani alisema. "Anapiga mpira kwa umakini mkubwa na anaweza kuupeleka pale anapopataka na anajua sana kufunga goli."

Uwezo huo wa kufunga ulitokeza mara mbili tu msimu uliopita katika msimu wake wa kwanza Milan, wakati alipocheza mechi 22 lakini sita tu kati ya hizo akianza katika kikosi cha kwanza. Pia alishindwa kutengeneza ushirikiano mzuri uwanjani na Ibrahimovic. "Siri ni kumpasia tu mpira, vinginevyo anakuja juu," El Shaaraway alisema kuhusu Ibrahimovich.

Lakini kuondoka kwa Ibra kulifungua kipaji chake na sasa El Shaarawy ni mchezaji wa timu ya wakubwa ya taifa ya Italia, akicheza mechi yake ya kwanza wakati walipoikabili England na akafunga goli lake la kwanza dhidi ya Ufaransa. Ni bonge la staa sasa.

"Nilidhani itakuwa ni jambo rahisi kutovimba kichwa," alisema. "Lakini ni ngumu. Unapomuona mchezasoka, unajisemea: 'Kwanini wanajisikia?' Lakini inapokuwa ni wewe, na watu hawaachi kukuomba uwasainie vijitabu vyao vya kumbukumbu, na daima wanakufuata, unaanza kujisikia wewe ni mtu fulani bab'kubwa. Bahati, baba yangu yupo karibu kuhakikisha natulia na kucheza mpira tu. Bado niko wa kawaida kwa watu wote, wakiwamo rafiki zangu wa zamani kutoka Savona. Tofauti pekee sasa ni kwamba ni mimi ndiye ninayenunua pizza."

Hakika, kitu pekee kilichobadilika ni jina la mshambuliaji wa Milan. Hata "la cresta" (kiduku chake) kimevumiliwa.

"[Silvio Berlusconi] aliniambia naweza kuendelea kunyoa staili yangu (ya kiduku)," El Shaarawy alisema.

No comments:

Post a Comment