Thursday, October 11, 2012

RIPOTI YA KAMATI YA NCHIMBI KUHUSU MAUAJI YA MWANGOSI YAUMBULIWA VIBAYA NA TUME YA UTAWALA BORA NA HAKI ZA BINADAMU YA JAJI AMIR MANENTO... RPC WA IRINGA MICHAEL KAMUHANDA, MSAJILI WA VYAMA JOHN TENDWA WABAINIKA KUVUNJA KATIBA NA SHERIA ZA NCHI KUELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI WA CHANNEL TENJaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento akionyesha ripoti ya Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Msajili wa Vyama vya siasa, John Tendwa.
Michael Kamuhanda, RPC wa Iringa
Mwangosi akishambuliwa na rundo la Polisi kabla ya kuuawa kwa bomu.

Polisi wakionekana pembeni ya mabaki ya mwili wa marehemu Mwangosi

Mabaki ya mwili wa Mwangosi yakionekana huku aliyeketi akiwa ni polisi aliyejeruhiwa pia na bomu lililomuua.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi.
Kajubi Mukajanga wa MCT (kulia) akionyesha ripoti ya mauaji ya Mwangosi juzi. Kushoto ni Mhariri wa gazeti la NIPASHE aliyekuwa akiwakilisha Jukwaa la Wahariri, Jesse Kwayu. 
SIKU moja baada ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, kutoa ripoti yenye ‘makengeza’ kuhusu Jeshi la Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imejiridhisha kuwa jeshi hilo lilivunja haki za binadamu, ikiwamo Kamanda wake wa Mkoa huo, Michael Kamuhanda, kukiuka misingi ya utawala bora, katika kuendesha operesheni iliyosababisha mauaji ya mwanahabari huyo, kinyume cha Katiba na sheria za nchi.

Vilevile, Tume hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Kiongozi mstaafu, Amiri Manento, pia imebaini kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alikiuka misingi ya utawala bora kwa kutoa maelekezo yanayokinzana na Sheria ya Takwimu namba 1 ya mwaka 2002.

Ripoti ya Tume hiyo iliwekwa hadharani na Jaji Manento, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Jaji Manento alizitaja haki za binadamu zilizovunjwa na jeshi hilo wakati wa operesheni yake hiyo kuwa ni pamoja na haki ya kuishi; haki ya kutoteswa na kutopigwa; haki ya usawa mbele ya sheria; na haki ya kukusanyika na kutoa maoni.

Alisema haki hizo za binadamu zinalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki ya Kiraia na Kisiasa na Mkataba wa Mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu.

Alisema ili kuwako utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.

Hata hivyo, alisema uchunguzi umebaini kuwa Kamanda Kamuhanda Septemba 2, mwaka huu, katika utekelezaji wa majukumu yake, alikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11 (a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura 322).

Jaji Manento alisema Kamanda Kamuhanda alikiuka sheria hizo kwa kuingilia kazi za Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za Chama cha Demoklrasia na Maendeleo (Chadema) wakati yeye (Kamuhanda) hakuwa kiongozi wa polisi wa eneo husika.

“Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” alisema Jaji Manento.

Kwa mujibu wa Jaji Manento, wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Chadema katika Kata ya Nyololo, Wilaya ya Mufindi ukiendelea, Kamanda Kamuhanda alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa Chadema wakamatwe, hali iliyowafanya wafuasi wa chama hicho kupinga kukamatwa kwa viongozi wao.

Jaji Manento alisema mbali na kutoa amri hiyo, Kamanda huyo aliamuru pia kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi la Chadema.

Aidha, alisema hatua ya Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora, kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yalikinzana na Sheria ya Takwimu namba 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa.

Alisema hatua hiyo ya Tendwa pia ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11 (a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa.

Jaji Manento pia alisema Ibara ya 8 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea kwamba, Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii.

Alisema pia ibara ya 18 (b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

“Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo, Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa Chadema walizuiwa na polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa,” alisema Jaji Manento na kuongeza:

“Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.”

Alisema baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo na kwamba, marehemu Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na kufa papo hapo.

Jaji Manento alisema Mwangosi aliuawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo ofisi ya Chadema tawi la Nyololo.

Alisema katika tukio hilo, wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, akiwamo mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE, Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chadema Wilaya ya Mufindi, Winnie Sanga, na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba, aliyekuwa akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Mwangosi.

“Kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililosababisha kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,” alisema Jaji Manento.

Alisema Chadema ni chama cha siasa, ambacho kina usajili wa kudumu na kwamba, chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vyenye usajili wa kudumu vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa ofisa wa polisi wa eneo husika.

Jaji Manento alisema baada ya taarifa kutolewa, chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi.

MAONI NA MAPENDEKEZO

Aliitaka Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya kuwa makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.

Pia kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.

Pia aliwatakwa viongozi wa Chadema na wafuasi wao kuepuka malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.

Alisema pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Pia alilitaka Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa kuepuka kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya Chadema kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa kampeni huko Zanzibar,” alisema Jaji Manento na kuongeza:

“Rai ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku Chadema walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo."

Pia alitaka demokrasia ya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa na elimu ya vyama vya siasa na sheria ya polisi kuhusu vyama hivyo itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.

WANAHARAKATI WAPONDA RIPOTI

Wanaharakati wameponda ripoti ya Kamati ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi iliyowasilishwa juzi na mwenyekiti wake, Jaji Stephen Ihema, na kusema kuwa yanatia aibu kwa jamii.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alitoa maoni hayo jana katika maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema matokeo yaliyotangazwa juzi na Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emanuel Nchimbi kuchunguza chanzo cha kifo hicho ni ya hovyo kwa kuwa yameonyesha namna ambavyo polisi wanavyolindana.

Alisema jamii yote inajua namna polisi ilivyohusika kumuua Mwangosi, lakini anashangaa kusikia matokeo ya uchunguzi yakiwaweka kando.

Ingawa alisema hajasoma ripoti kamili ya kamati hiyo, lakini alisema kwa matokeo hayo yanatia wasiwasi na kwamba picha zilizoonyesha tukio lile zilitoka wapi.

Alisema kesho kituo chake kinatarajia kutoa msimamo kamili juu ya tukio hilo la kinyama ambalo lilifanywa na polisi.

Ripoti ya jana ya Tume ya Utawala Bora ni ya tatu kuwekwa hadharani. Ya kwanza ilikuwa ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri (TEF) ambayo iliwaona polisi kuwa wahusika wakuu wa mauaji hayo huku RPC Kamuhanda akielezwa kuwa alisimamia mauaji hayo moja kwa moja.

Ripoti ya MCT na TEF ilitolewa siku moja na ya Kamati ya Waziri Nchimbi, zikikubalina kuwa kulikuwa na uhusiano mbaya baina ya waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa na polisi, lakini ile ya kwanza (MCT na TEF) ikithibitisha kuhusika kwa polisi katika mauaji wakati ya Waziri Nchimbi ikikwepa ukweli huo. Soma Muhtasari wa Ripoti ya Tume ya Utawala Bora na Haki za Binadamu uk. 14.

No comments:

Post a Comment