Monday, October 29, 2012

MTANZANIA SAID MBELWA APIMA UZITO LEO NA MPINZANI WAKE HAMID RAHIMI AMBAYE NI BINGWA WA DUNIA WA UZITO WA KATI ANAYETAMBULIWA NA WBU.... NI PAMBANO LA KIHISTORIA KUWANIA MKANDA WA AMANI WA UZITO WA KATI WBO LITAKALOFANYIKA JIJINI KABUL, AFGHANISTAN KESHO... MBELWA AAHIDI KUSHINDA KWA KO RAUNDI YA NNE... RAHIMI AAHIDI KUSHINDA 'KO' KATIKA RAUNDI YA 3

Bingwa wa Dunia wa uzito wa kati anayetambuliwa na World Boxing Union (WBU), raia wa Afghanistan Hamid Rahimi (kushoto) na mpinzani wake kutoka Tanzania, Said Mbelwa, wakijiandaa kupima rasmi uzito mjini Kabul leo Oktoba 29, 2012, kabla ya pambano lao la ngumi la kimataifa kuwania mkanda wa amani (Fight 4 Peace) WBU litakalofanyika kesho Jumanne. (Picha: REUTERS)
Lazima nimtoe nishai...! Said Mbelwa akitambiana na bingwa wa dunia wa uzito wa kati anayetambuliwa na WBU, Hamid Rahim wakati wakipima uzito leo Oktoba 29, 2012 kabla ya pambano lao la kuwania mkanda maalum wa amani kesho mjini Kabul. (Picha: Reuters)
Hamid na Mbelwa wakitambiana mbele ya waandishi wa habari baada ya kupimwa uzito leo Oktoba 29, 2012 mjini Kabul huku kila mmoja akitamba kutwaa mkanda maalum wa amani unaotambuliwa na WBU unaoonekana nyuma yao. Pambano hilo litafanyika kesho mjini Kabul.
Bingwa wa Dunia wa uzito wa kati anayetambuliwa na World Boxing Union (WBU),  raia wa Afghanistan Hamid Rahimi akitunisha msuli huku akiwa amesimama kwenye mzani wakati wa upimaji rasmi wa uzito mjini Kabul leo Oktoba 29, 2012. Rahimi atatwangana na Said Mbelwa wa Tanzania kesho Jumanne katika pambano lao la ngumi la kimataifa la kuwania mkanda wa amani liitwalo "Fight 4 Peace" litakalofanyika mjini Kabul. (Picha: REUTERS)



Mleteni huyo bingwa wenu wa dunia...! Bondia kutoka Tanzania, Said Mbelwa akitunisha misuli yake wakati wakipima uzito leo mjini Kabul, Afghanistan kabla ya pambano lake dhidi ya Hamid Rahim litakalofanyika kesho Jumanne Oktoba 30, 2012. (Picha: REUTERS)





Bingwa wa Dunia wa uzito wa kati anayetambuliwa na WBU, bondia Hamid Rahim (katikati) akipokewa na maelfu ya mashabiki mjini Kabul juzi wakati akitokea Ujerumani kujiandaa na pambano lake la kuwania mkanda maalum wa amani wa WBU dhidi ya Mtanzania Said Mbelwa.

Mtanzania Said Mbelwa akitua mjini Kabul kujiandaa na pambano lake la uzito wa kati kuwania mkanda maalum wa amani dhidi ya bingwa wa dunia anayetambuliwa na WBU, Hamid Rahim. Pambano hilo litafanyika mjini Kabul, Afghanistan kesho Jumanne, Oktoba 30, 2012.  
KABUL, Afghanistan
BONDIA wa kimataifa kutoka Tanzania, Said Mbelwa ameahidi kumchapa kwa K.O bingwa wa dunia wa uzito wa kati (WBU) mwenye uraia wa Ujerumani na Afghanistan, Hamid Rahimi wakati watakapokutana kesho katika pambano lao la kuwania mkanda maalum wa amani unaotambuliwa na WBU jijini Kabul, Afghanistan.


Akizungumza mara baada ya kutua jijini Kabul kwa ajili ya pambano hilo la kwanza la kulipwa kuwahi kufanyika nchini Afghanistan, Mbelwa alisema kuwa amejiandaa vya kutosha kumchapa mpinzani wake katika raundi ya nne tu ya pambano hilo litakalofuatiliwa na maelfu ya watu ulimwenguni kote. 


Mbelwa alisema kuwa hakusafiri maelfu ya kilomita kutoka Tanzania hadi Afghanistan bure bure, bali kumchapa Rahimi katika pambano hilo la ‘Fight 4 Peace.’


“Nampa Hamid Rahimi na timu yake pongezi za pekee kwa kuandaa pambano hili,” amesema Mbelwa.


“Natambua kwamba hili ni tukio la kihistoria nchini Afghanistan na pia linabeba ujumbe muhimu sana kwa watu wote duniani. Lakini mara tu baada ya kengele ya kuanza pambano kupigwa ulingoni, litakuwa ni pambano kali la ngumi kama yalivyo mapambano mengine. Na ninawaahidi kwamba lazima nitashinda. Nimejiandaa vizuri sana na ninaamini nitamchapa Rahimi kwa KO katika raundi ya nne,” amesema Mbelwa.


Hata hivyo, wakati Rahimi mwenye uraia wa nchi za Ujerumani na Afghanistan na kocha wake Balu Sauer waliposikia tambo za Mbelwa, walitoa jibu rahisi kwa kusema kuwa wamefurahi kusikia 'mkwara' huo na kwamba wao wamejiandaa kushinda mapema zaidi dhidi ya Mtanzania huyo. 


“Ni vizuri kusikia kwamba anataka kumshinda Rahimi kwa KO katika raundi ya nne,” amesema Sauer wakati wa mkutano na waandishi wa habari.


“Hii inamaanisha kuwa tunapaswa kubadili mipango yetu ya pambano hili, Rahimi atalazimika kuwa wepesi zaidi yake kwa kumchapa mapema kwa KO katika raundi ya tatu tu. Hivyo ndivyo itakavyokuwa,” ameongeza Sauer.


Pambano hilo la “Fight 4 Peace” kati ya Rahimi na Mbelwa linafanyika kesho na mshindi atakabidhiwa taji lililo wazi sasa la WBO litakaloitwa “bingwa wa amani”, ambalo ni maalum kwa tukio hilo.

RAIS HAMID KARZAI
Rahimi na timu yake walipata mapokezi ya kifalme kutoka kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi wa Afghanistan mjini Kabul baada ya kutua mjini humo Ijumaa kujiandaa na pambano hilo la kesho  litakalokuwa la raundi 12.

Rahimi aliyealikwa na Kamati ya Olimpiki ya Afghanistan na asasi nyingine binafsi kadhaa, alifanya mkutano na waandishi wa habari na pia kuhojiwa na TV mbalimbali kabla ya kualikwa kwenda ikulu ambako alifanya mazungumzo na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai.


“Nimefurahi sana kurejea nchini mwangu na kupigania uhuru na amani”, amesema Rahimi.


Shirika la Ngumi Duniani (WBO), linamuunga mkono Rahimi na mpango wake wa kuleta amani nchini Afghanistan na lilitangaza kumuunga mkono bingwa huyo wa dunia wa WBO kwa hali na mali wakati wa mkutano wa mwaka uliofanyika wiki hii mjini Hollywood, Florida nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment