Tuesday, September 4, 2012

SOMA KISA CHA CRISTIANO RONALDO KUANZA KUZINGUANA NA KLABU YAKE REAL MADRID…!

Ronaldo

Dah... nini tena?
MADRID, Hispania
CRISTIANO Ronaldo anataka Real Madrid kumpa mkataba mpya utakaomuingizia paundi za England milioni 25 (Sh. bilioni 62) kwa mwaka.

Straika huyo ambaye hivi sasa hana furaha tena klabuni hapo ana “usongo” wa kutaka kuanza mazungumzo mapya yatakayomfanya asaini mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka sita, licha ya kwamba hivi sasa bado amebakiza miaka mitatu kumaliza mkataba wake.

Ronaldo, 27, analipwa mshahara wa paundi za England milioni 9.6 (Sh. bilioni 24) kwa mwaka, lakini kutokana na mabadiliko ya sheria za kodi za Hispania, sasa kiasi cha mshahara anaokwenda nao nyumbani baada ya makato kimepungua na kufikia paundi za England milioni 7.2. (Sh. bilioni 18)

Hivi sasa anataka alipwe mshahara utakaomfanya aende nyumbani kwake na paundi za England milioni 12 (Sh. bilioni 30) kwa mwaka. Kwa madai yake hayo mapya, hata kwa sheria ya awali ya kodi, itamaanisha kwamba sasa straika huyo alipwe malipo ghafi (ya kabla ya kodi) kiasi cha paundi za England milioni 14.5 (Sh. bilioni 36) kwa mwaka.

Tatizo la Real Madrid kwa sasa ni kwamba, ndani ya miaka miwili, kiwango cha kodi atakacholipa Ronaldo kitapanda kutoka asilimia 24 hadi 52.

Na hilo linamaanisha kwamba ili (Ronaldo) alipwe kiasi anachotaka baada ya kukatwa kodi cha paundi za England milioni 12 (Sh. bilioni 30) kwa mwaka, mshahara wake wa jumla kabla ya kodi unapaswa kuwa takriban paundi za England milioni 25 (Sh. bilioni 62) kwa mwaka, sawa na paundi za England 480,000 (Sh. bilioni 1.2) kwa wiki!

Ronaldo amekuwa akitaka asainishwe mkataba mpya tangu Januari.

Hata hivyo, wakuu wa Real Madrid wamekuwa wakipinga kiwango anachotaka na pande hizo zimekuwa katika mazungumzo, hasa ikifahamika wazi kwamba kanuni mpya inayozibana klabu juu ya ukomo wa matumizi ya fedha ya UEFA ikitarajiwa kuanza kutumika miaka miwili ijayo.

Ronaldo bado hajawasilisha maombi rasmi ya kutaka aongezewe mshahara, lakini wapambe wake wanaamini kuwa anastahili kupewa mkataba mnono kuliko wa mwanasoka yeyote duniani na kuipiku mikataba iliyosainiwa na mastraika Didier Drogba na Nicolas Anelka wanaochezea klabu za Shenhua Shanghai nchini China.

Hadi sasa ameshafunga mabao 150 katika mechi 149 za michuano yote tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Manchester United miaka mitatu iliyopita, huku pia akiwa na rekodi ya kushangaza ya kufunga mabao 114 katika mechi 104 za La Liga, Ligi Kuu ya Hispania alizochezea klabu hiyo iliyomnunua kwa paundi za England milioni 80 (Sh. bilioni 197).

Na bado pia thamani yake hailipiki kulinganisha na “mihela” anayoiingizia klabu ya Real Madrid kupitia mauzo ya bidhaa mbalimbali na udhamini.

Straika huyo nyota wa kimataifa wa Ureno ana kipengele ghali cha kuvunja mkataba wake cha paundi za England milioni 791 (Sh. trilioni 2) lakini kwa kufichua kwamba hana furaha baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wao wa Jumapili wa mabao 3-0 dhidi ya Granada, amefungua milango ya uwezekano wa kuhama katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.

Hata hivyo, kumuuza Ronaldo bado kunaonekana kuwa ni uamuzi usiopewa nafasi kwa sasa, lakini linaweza kutokea.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa uhusiano wa Ronaldo na baadhi ya wachezaji wenzake katika chumba cha kuvalia pia hautabiriki.

Inadaiwa kwamba kuna msuguano kati ya wachezaji wanaozungumza Kireno — Ronaldo, Pepe, Marcelo, Fabio Coentrao  — na wanaozungumza Kihispaniola, hasa nahodha Iker Casillas na Sergio Ramos.


Alipozungumza na waandishi baada ya mechi dhidi ya Granada, Ronaldo alisema: “Sina furaha na watu wa ndani ya klabu wanajua kuhusiana na hili. Hii ndiyo sababu kwanini sishangilii. Ni suala la kikazi. Siwezi kulizungumzia zaidi.”

No comments:

Post a Comment