Sunday, September 9, 2012

RYAN GIGGS: NIMEAMINI...ROBIN VAN PERSIE NI BALAA!

Straika Robin Van Persie
Winga Ryan Giggs
MANCHESTER, England
Winga Ryan Giggs anaamini kwamba usajili "bab'kubwa" waliofanya  Manchester United kwa kumnasa straika Robin van Persie utaisaidia timu yao katika mbio za kuwania taji la 20 la Ligi Kuu ya England msimu huu.

Man U walipoteza ubingwa msimu uliopita kwa  'majirani wenye kelele' Man City kwa tofauti ya mabao, lakini winga huyo wa kimataifa wa Wales anaamini kwamba ujio wa Van Persie utawabeba, ikiwa ni baada ya straika huyo kupachika mabao 30 katika Ligi Kuu wakati akiichezea Arsenal msimu uliopita.

Uhamisho wa Van Persie mwenye miaka 28 ulioigharimu Man U dau la paundi za England milioni 22 ulimaanisha mabadiliko ya sera za hivi karibuni za kocha  Alex Ferguson ambaye huwekeza zaidi kwa yosso wenye vipaji, lakini Giggs anaamini kwamba ni lilikuwa "dili" safi baada ya straika huyo wa zamani wa Arsenal kufikisha mabao manne katika mechi tatu tu alizoichezea Man U tangu atue msimu huu.

Giggs ameiambia Sky Sports News: "Mabo aliyofunga (Van Persie), na kiwango chake kwa ujumla, ni wazi kwamba yeye ni mchezaji wa kiwango cha dunia.

"Sera za kocha katika kipindi cha miaka 10 na 15 iliyopita zilikuwa ni kununua wachezaji yosso na kuwaendeleza, kama ilivyokuwa kwa Cristiano (Ronaldo) na Wayne (Rooney).

"Lakini Robin tayari ni nyota wa kiwango cha dunia na ameshathibitisha hilo. Nadhani ameonyesha hayo katika mechi chache za mwanzo wa msimu na ninaamini kuna mengi yanakuja."

Kushindwa katika mechi ya mwisho wa msimu kwa mahasimu wao wa jadi, Manchester City lilikuwa pigo kubwa kwa kikosi cha Man U, na Giggs anaamini kwamba kuongezwa kwa 'muuaji' huyo wa Uholanzi kunaweza kuonyesha tofauti baina yao kama klabu hizo mbili za Manchester zitachuana tena vikali kama msimu uliopita.

"Tulishindwa kwa tofauti ya mabao, kwa hiyo ni matumaini yetu kwamba kutokana na magoli anayoleta, kama litakuja suala la tofauti ya mabao, basi safari hii sisi nd'o tutakaoibuka vinara."

No comments:

Post a Comment