Wednesday, September 5, 2012

KUJISAJILI KWA NJIA YA SIMU EPIQ BSS MWISHO SEPT. 13

Washindi wa Shindano la Epiq Bongo Star Search Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na majaji wa shindano hilo Ritha Poulse aliyechuchumaa (kushoto), Master Jay (aliyechuchumaa kulia) na Salama Jabir aliyesimama kulia.
Washindi wa Shindano la Epiq Bongo Star Search Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja.


WAPENZI wa muziki wenye shauku ya kujiunga na washindi 20 wa shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS) watakaoingia kambini hivi karibuni wametakiwa kutumia fursa pekee iliyobakia itakayowawezesha kutimiza ndoto zao hizo.


Fursa hiyo ni kufanya usaili kwa njia ya simu, njia ambayo inatoa fursa kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kuonesha vipaji vyao katika usaili pamoja na wale ambao walionesha vipaji vyao lakini hawakuchaguliwa wakati wa usaili wa shindano hilo.


Akizungumzia njia hiyo, Jaji Mkuu wa EBSS 2012, Ritha Paulsen alisema kuwa Septemba 13 ndio itakuwa mwisho wa kutumika kwa njia hiyo ya kutafutia vipaji hivyo aliwataka watu kuitumia njia hiyo mapema iwezekanavyo kuonyesha vipaji vyao.


“Utaratibu huu wa kufanya usaili kwa njia ya simu uliwekwa maalumu kwa watu wanaotaka kujaribu bahati zao tena baada ya kushindwa kupita kwenye usaili mara ya kwanza, au wale ambao hawakupata kabisa fursa ya kuwaona majaji, aidha kwa sababu hawakuwafikia mikoani kwao, au hawakuweza kufika kwenye usaili kwa sababu zozote zile,” alisema Rita.


Aliongeza kuwa mpaka sasa watu wengi wamefanya usaili kwa njia hiyo na pia aliwataka watu kujitokeza zaidi kuwania nafasi hiyo ambayo itawapatia fursa ya kuungana na wengine 20 wataokaoingia kwenye jumba la EBSS mwaka huu.


"Mwamko ni mkubwa sana kuliko hata tulivyotarajia, watu wengi sana wamepiga simu kufanya usaili, na tunawahamasisha waendelee ili kupata nafasi ya kujishindia Sh. milioni 50," alisema Ritha.


Kwa upande wake Afisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, alisema dhumuni la kampuni yao ni kuifanya EBSS kuwa shindano la kimataifa lakini pia kumpa fursa kila mwenye kipaji kufikiwa.


”Lengo la kuu la EBSS ukiachilia mbali kutoa burudani ni kuhakikisha kuwa tunaboresha maisha ya vijana wanaojiunga na shindano hilo, lakini hiyo inaanza kwa kuwapa nafasi wote, hata wale ambao shindano hili halikuwafikia mikoani mwao," alisema Khan.


Vijana wanaotaka kushiriki usahili kwa njia ya simu wanaweza kupiga namba 090155100 ambapo watapatiwa maelekezo ya namna ya kurekodi sauti zao na kisha zitasikilizwa na majaji.


Shindano hilo ambalo linaonyeshwa kila Jumapili saa 3:30 usiku kupitia kituo cha televisheni cha ITV, linatoa fursa ya kipekee pia kwa wapenzi wa shindano kujua kinachoendelea kwenye shindano hilo kwa kupitia simu zao za mikononi kwa kutuma ujumbe EBSS kwenda namba 15530.

No comments:

Post a Comment