Thursday, September 13, 2012

DIAMOND PLATNUMZ KUFANYA USAILI WA KUSAKA WATAKAOONEKANA KATIKA VIDEO YAKE MPYA

Diamond Platnumz

Diamond Platnumz

MSANII wa kimataifa wa Tanzania, Naseeb Abdul a.k.a Diamond Platnumz, anatarajia  kufanya usaili kwa ajili ya watu watakaotumika katika kurekodi video ya wimbo wake mpya ambao utaachiwa hivi karibuni.

Mkurugenzi wa kampuni ya One Touch Solutions, Petter Mwendapole alisema mjini Dar es Salaam kuwa Diamond amefikia uamuzi huo katika kuhakikisha kazi zake zinafanyika katika kiwango cha kimataifa.

“Jumamosi ijayo tutafanya usaili wa watu ambao wataonekana kwenye video hiyo, hii ni mara ya kwanza kwa kitu kama hiki kufanyika nchini kwetu ingawa wenzetu Ulaya wamekuwa wanafanya hivyo na wanaonekana wanakuwa wanalipwa tofauti na video nyingi za wasanii wa hapa kwetu na hao watakaochaguliwa kwenye video hiyo watalipwa pia,” alisema.

Akizungumzia kuhusu video hiyo, Mwendapole alisema itarekodi ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya soko ambalo msanii huyo analiangalia kwa sasa huku video hiyo ikifanya na kampuni bora kabisa Tanzania.

Kwa upande wake Diamond alisema lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuleta mapinduzi katika sekta ya muziki nchini lakini pia kutengeneza ajira kwa ajili ya wasichana na wavulana ambao wako mitaani lakini wanapenda muziki.

Diamond ambaye alikuwa nchini Marekani wiki iliyopita anatarajiwa tena kwenda Marekani kwa ajili ya onyesho moja la muziki.

Msanii huyo alifanya mapinduzi katika medani ya muziki wa bongo baada ya kufanya onyesho lake alilolipa jina la Diamond’s are Forever pale Mlimani City ambapo katika shoo hiyo aliifanya mwenyewe na kiingilio kikiwa sh 50,000 jambo ambalo halijawahi kufanyika katika ulimwengu wa muziki nchini na alipata kukaririwa akisema kwamba onyshio hilo lilimuingizia Sh. milioni 100.

No comments:

Post a Comment