Saturday, August 25, 2012

XAVI: BARCELONA TUTAWACHAPA TENA REAL MADRID NA KUBEBA TAJI LA SUPER COPA JUMATANO

Nimewaziba mdomo na pua...! Xavi wa Barca akishangilia goli alilofunga dhidi ya Real Madrid wakati wa mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa kwenye Uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona, Alhamisi.  
Natishaaaa...! Xavi akishangilia goli lake dhidi ya Real Madrid wakati wa mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa kwenye Uwanja wa Camp Nou, Alhamisi.
BARCELONA, Hispania
GOLI la Xavi dhidi ya Real Madrid katika mechi yao ya kwanza ya kuwania taji la Super Copa limeihakikishia Barcelona faida ya goli moja kabla ya mechi yao ya marudiano kwenye Uwanja wa Bernabeu, na kiungo huyo wa timu ya taifa ya Hispania anaamini kwamba watashinda tena na kumpa kocha wao mpya, Tito Vilanova kombe la kwanza tangu aanze kazi ya kuwaongoza.

Barca walilazimika kwanza kusawazisha baada ya kutanguliwa kutokana na goli la kichwa la Cristiano Ronaldo, na Xavi alipongeza uwezo waliouonyesha Barcelona wa kurudi mchezoni haraka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Xavi amesema: "Tulianza mechi vizuri, lakini  tulionyesha ungangari pia kwa kurudi mchezoni.

"Tulicheza soka safi, na kushinda ilikuwa muhimu kwani imemaanisha kuwa sasa tunajua ni kitu gani cha kufanya tukiw akwenye Uwanja wa Bernabeu. Ikiwa tutacheza vilevile tukiwa Madrid (kama tulivyofanya kwenye Uwanja wa Camp Nou) basi kombe tutalibeba."

Xavi pia ametoa kauli ya kumfariji Victor Valdes, ambaye makosa yake kuelekea mwisho wa mechi yao ya kwanza iliyochezwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Camp Nou yalimzawadia Angel Di Maria goli rahisi kabisa ambalo limeifanya mechi hiyo iendelee kuwa ngumu kutokana na ushindi mwembamba wa 3-2 walioupata Barcelona wakiwa nyumbani.

"Victor (Valdes) ni mchezaji wa kulipwa na tena ni kipa bora kabisa tunayemhitaji," aliongeza Xavi.

Zote, Real Madrid na Barcelona zitarudi katika La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa kucheza kesho kabla mahasimu hao wa jadi hawajarudiana Jumatano katika mechi yao ya 'el clasico' kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu jijini Madrid.

No comments:

Post a Comment