Monday, August 6, 2012

PREZZO AZIKOSA SH. MILIONI 460 ZA BIG BROTHER

*Mzigo wabaki Afrika Kusini kwa Keagan
Keagan wa Afrika Kusini "akilipua" shampeni baada ya kutangazwa mshindi wa Dola 300,000 (sawa na Sh. milioni 460) za Big Brother StarGame 2012
Prezzo
Keagan wa Afrika Kusini akisindikizwa kuelekea stejini baada ya kutangazwa mshindi wa Big Brother StarGame 2012
Keagan wa Afrika Kusini

Na Amour Hassan
RAPA wa Kenya, CMB Prezzo ameibuka mshindi wa pili wa shindano la Big Brother StarGAME 2012 huku akimshuhudia kijana wa nyumbani Keagan akizibakisha kwa mara ya kwanza dola 300,000 (sawa na Sh. milioni 460) nchini Afrika Kusini.

Washiriki sita walikuwa wamebaki ndani ya nyumba hadi leo siku ya 91 na ya mwisho ya shindano hilo ambao ni Kyle wa Uganda, Wati (Malawi), Lady May (Namibia), Talia (Zambia), Prezzo na Keagan.

Wati alitangulia kutolewa, akafuatia Kyle, Talia, Lady May na wakabaki wawili tu ndani ya jumba Prezzo na mwenyeji wa mashindano, Keagan.

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu huku burudani zikiendelea nje ya jumba, mtangazaji wa shoo hiyo, IK, alirejesha kamera ndani ya nyumba na baada ya kuwaweka roho juu washiriki hao wawili ikiwa ni pamoja na kuwataka waseme maneno yao ya mwisho shindanoni, baadaye akamtangaza Keagan kuwa ndiye mshindi.

Prezzo hakupoteza muda wala hakukumbuka kwenda kumpongeza mwenzake, alitoka moja kwa moja nje ya jumba, ambako alipokewa na nderemo za mashabiki waliojaa pamoja na mtangazaji IK.

Huku akijitahidi kuzuia machozi yasitoke, 'The Prezident himself' Prezzo aliulizwa kama ataendeleza mapenzi yake na muimbaji wa Nigeria, Goldie, kama walivyokuwa mjengoni, alijibu: "Tusibiri tuone."

Kisha Prezzo aliambiwa kuwa hataondoka mtupu kwa sababu kura za mashabiki zimemchagua kuwa balozi wa kampeni ya ONE ambayo inawajumuisha mastaa kama rapa Nas, Mary J. Blige wa Marekani na wengine wengi.

"Mbali na hiyo pia umealikwa kwenda kuhudhuria shoo ya Jay Z Marekani," alisema IK kumweleza Prezzo.

IK pia aliwaambia washiriki wengine walioshika nafasi tano za kwanza: "Hamtaondoka mikono mitupu... mtapata PVR decoder, IPhone smartphone, na scooter."

Licha ya ushindi, Keagan alionekana kuwa mtulivu mno na hakushangilia, pengine alikuwa haamini kama sasa yeye ni tajiri wa Sh. milioni 460.


No comments:

Post a Comment