Friday, August 10, 2012

LYON YAMTANGAZA KOCHA MUARGENTINA


Na Somoe Ng'itu
KLABU ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo imemtangaza raia wa Argentina, Pablo Ignacio 'Velez' (38) kuwa kocha wake mkuu.

Ignacio aliwasili nchini Jumatano akitokea Hispania ambako alikuwa anaishi na kufanya kazi hiyo ya ukocha.

Akizungumza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa African Lyon, Rahim Kangezi 'Zamunda', alisema alisema kuwa wamesaini mkataba wa mwaka mmoja na kocha huyo lakini wanatarajia kufanya naye kazi kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kangezi alisema kuwa wameamua kuboresha benchi lao la ufundi kwa kumleta kocha huyo kwa sababu wanataka kuwapa nafasi wachezaji chipukizi wa hapa nchini kuonyesha vipaji vyao na hatimaye kuuzwa katika nchi za Ulaya.

"Tunataka tupige hatua ya maendeleo ndio maana tumemleta kocha huyo ambaye kikubwa kilichomfanya ajiunge na African Lyon ni kutimiza ndoto zake za kuja Afrika kufanya kazi na si kulipwa mshahara mkubwa," alisema mmiliki huyo wa African Lyon.

Ignacio ambaye anazungumza zaidi Kispaniola, alisema kwamba atakuwa na programu ya maendeleo ya muda mrefu wa kuiendeleza timu hiyo kwa kuwapa nafasi zaidi wachezaji chipukizi ambao wanapokea mafunzo haraka na kuonyesha vipaji vyao.

Alisema kwamba wachezaji wa timu hiyo aliokutana nao wameonekana kuwa na uwezo lakini wanakosa mbinu za kiufundi za uwanjani jambo ambalo ndio atalifanyia kazi.

Aliongeza kuwa ataanzisha programu maalumu ya timu ya vijana kuanzia umri chini ya miaka 14 na 17 ambao ndio wenye kuweza kuhimili ushindani uliopo na anaamini wachezaji wa umri chini ya miaka 20 wenye uwezo wanafaa kuuzwa Ulaya kama walivyo nyota wengine wa nchi za Afrika wanaocheza nje ya bara hili la Afrika.

Ignacio amekuwa ni kocha watatu wa kigeni mpya ambaye msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba Mosi ataongoza timu ya Ligi Kuu ya Bara.

Kocha huyo amewahi kufundisha klabu za daraja la kwanza za Banco de Cordoba na Club Atletico Argentino Periarol zote za Agentina.

Makocha wengine wapya ni wa mabingwa wa Kombe la Kagame, Mbelgiji, Tom Saintfiet na Mserbia, Boris Bonjak 'Boca" ambaye ametua Azam.

No comments:

Post a Comment