Tuesday, August 14, 2012

MOURINHO: KWA MAKOMBE NILIYOBEBA KATIKA LIGI TATU BORA DUNIANI, SASA MNAPASWA KUNITAMBUA KWA JINA JIPYA LA "THE ONLY ONE", SIO "THE SPECIAL ONE"


Jose Mourinho
MADRID, Hispania
Jose Mourinho anaamini kwamba anastahili kutambuliwa kwa jina la “Only one” badala ya “Special One”, baada ya kuwa kocha pekee aliyewahi kutwaa ubingwa katika ligi kuu kali zaidi zinazojulikana kama 'top 3' barani Ulaya.

Akizungumza katika televisheni ya Ureno ya SIC jana, Mourinho alieleza kwamba weledi wake katika kufundisha umeongezeka, na kwamba sasa amekuwa hajiangalii sana yeye na kwamba hafikirii sana kutwaa tuzo binafsi.

"Mambo yamekuwa yakiniendea vizuri sana, asante Mungu," alikiambia kituo hicho.

"Siku hizi nawafikiria wengine zaidi. Furaha ya kushinda nikiwa Inter Milan ilikuwa ni kuiona klabu hiyo, ambayo haikuwahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa miaka 50, ikibeba taji hilo.

"Hicho ndicho kinachonivutia mimi zaidi na zaidi, badala ya kuangalia mafanikio binafsi."

Mourinho alitwaa ubingwa wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita akiwa na klabu yake ya sasa ya Real Madrid, alitwaa mara mbili ubingwa wa Serie A, Ligi Kuu ya Italia akiwa na Inter, akabeba mara mbili pia taji la Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea na vilevile akatwaa mara mbili ubingwa wa Ligi Kuu ya Ureno akiwa na Porto. Zaidi ya mataji hayo, pia aliwahi kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa na Porto na Inter.

"Mnipende, msinipende... ni mimi tu ndiye niyetwaa ubingwa katika ligi kuu zote tatu zinazotajwa kuwa kali zaidi duniani. Kwa hiyo, badala ya kuniita 'Special One', watu sasa wanapaswa kuanza kuniita mimi kwa jina la 'Only One'," Mourinho alisema katika mahojiano yake yaliyorushwa hewani jana.

Kocha huyo wa Real Madrid alikuwa akifahamika kwa jina la utani la “The Special One” wakati akiwa England baada ya kujipachika jina hilo wakati akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kufuatia uhamisho wake kutoka Porto kwenda Chelsea mwaka 2004.

Real Madrid wataanza kampeni za kutetea ubingwa wao wa La Liga Jumapili kwa kucheza dhidi ya Valencia na Agosti 25 watavaana na Barcelona katika mechi yao ya kuwania taji la 'Super Cup'.

No comments:

Post a Comment