Thursday, August 16, 2012

FERGUSON ACHEKELEA UJIO WA ROBIN VAN PERSIE... ASEMA ATAMPANGA JUMATATU KATIKA MECHI YAO YA UFUNGUZI WA LIGI KUU YA ENGLAND DHIDI YA EVERTON

Van Persie ... anavyoonekana katika picha hii iliyofanyiwa utundu wa 'graphics' na mashabiki wa Man U

Van Persie ... hii pia ni picha iliyotengenezwa na mashabiki wa Man U
LONDON, England
KOCHA wa Manchester United, Alex Ferguson ana matumaini ya kumtumia straika wake mpya, Robin van Persie wakati watakapocheza mechi yao ya ufunguzi wa msimu wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Everton Jumatatu ikiwa Mholanzi huyo atafuzu vipimo vya uchunguzi wa afya.

"Tumeshakubaliana kuhusu ada ya uhamisho, ambayo sisi tumeridhishwa nayo," Ferguson amesema leo kupitia tovuti ya Man U (www.manutd.com).

Straika huyo wa kimataifa wa Uholanzi alisajiliwa kutoka Arsenal jana kwa ada ya uhamisho inayotajwa kuwa ni paundi za England milioni 24 (Sh. bilioni 60).

"Yuko njiani kuja hapa (Manchester) akitokea London kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya baadaye. Natumaini kwamba kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa. Tunatumaini atakuwa tayari kucheza Jumatatu usiku," ameongeza Ferguson.

"Tumefurahi kuona mchezaji wa kiwango cha juu kama Robin van Persie akija katika timu yetu. Nimefurahi sana."

Van Persie alifunga magoli 37 msimu uliopita wakati Arsenal ikimaliza ya tatu katika ligi kuu ya England na pia kufika katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Arsenal, hata hivyo, imeshindwa kuongeza akiba ya makombe yao tangu walipotwaa Kombe la FA mwaka 2005 kufuatia ushindi wa penati katika fainali waliyocheza dhidi ya Man U.

No comments:

Post a Comment