Sunday, August 26, 2012

ARSENAL NA DALILI ZA MWAKA MWINGINE WA TAABU ... AKINA PODOLSKI, GIROUD WAPIGA MASHUTI 16 BILA GOLI KATIKA MECHI WALIYOTAWALA YOTE DHIDI YA STOKE LEO

Kweli huu tena ni mwaka wa taabu...! Kocha Arsene Wenger (kulia) anavyoonekana wakati akizungumza na mwamuzi msaidizi wa nne, Howard Webb wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Britannia leo Agosti 26, 2012. (Picha: Reuters)

Tulia weweee...! Mikel Arteta wa Arsenal (kushoto) akichuana na Michael Kightly wa Stoke City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Britannia leo Agosti 26, 2012. (Picha: Reuters)

Yalaaaa...! Aaron Ramsey wa Arsenal (kushoto) akichuana na Wilson Palacios wa Stoke City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Britannia leo Agosti 26, 2012. (Picha: Reuters)
LONDON, England
Stoke City na Arsenal zilionekana kukosa makali mbele ya lango wakati zikimaliza mechi yao kwa sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Britannia na kuziacha zikihaha kupata ushindi wa kwanza baada ya zote kupata sare pia katika mechi zao za ufunguzi wa Ligi Kuu ya England wiki iliyopita.

Arsenal, waliotoka sare ya 0-0 dhidi ya Sunderland wiki iliyopita, walikaribia kupata goli katika dakika za majeruhi wakati straika wa Ufaransa, Olivier Giroud alipopiga shuti kali kutoka umbali wa mita 40 ambalo hata hivyo lilipaa juu ya lango.

Hata hivyo, Giroud alionekana kuwa angefanya vizuri zaidi kama angempasia Aaron Ramsey aliyekuwa peke yake katika nafasi nzuri na pengine angeweza kufunga kirahisi.

Stoke, walioanza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Reading wiki iliyopita, walikaribia pia kupata goli kutokana na jitihada za Peter Crouch, lakini mechi hiyo ikamalizika kwa sare ya 0-0 licha ya Arsenal kutawala muda wote, wakipiga mashuti 16 kuelekea langoni dhidi ya manne ya Stoke.

Sare isiyo na bao ya pili mfululizo si mwanzo mzuri kwa Arsenal ambayo inasaka taji la kwanza msimu huu baada ya ukame wa misimu saba! 

No comments:

Post a Comment