Monday, July 30, 2012

MESSI: MAPUMZIKO YAMENIONGEZA MAKALI

Lionel Messi akishangilia moja ya mabao yake...

NYOTA wa Barcelona, Lionel Messi anajisikia kama mtu mpya baada ya kupata mapumziko adimu ya mwisho wa msimu bila ya kuwa na michuano yoyote.

Mwanasoka Bora wa Dunia Messi alikuwa na kibarua cha kuichezea timu yake ya taifa ya Argentina katika michuano ya Copa America na Kombe la Dunia katika mapumziko ya mwisho wa msimu kwa miaka miwili iliyopita, pamoja na Olimpiki za mwaka 2008, na anaamini mapumziko kamilifu aliyoyapata mara hii yatamlipa katika wakati msimu wa 2012-13 utakapoanza.


Messi alifunga 'hat trick' katika ushindi wa 8-0 kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Raja Casablanca nchini Morocco usiku wa kuamkia Jumapili.


Aliliambia gazeti la El Mundo Deportivo, "Sijacheza vyema mechi za maandalizi ya msimu mpya kwa muda mrefu sana kwa sababu daima nawasili nikiwa nimechelewa. Ni jambo zuri sana kuwa na mapumziko marefu kiasi kile."


Messi anaamini mabadiliko ya kocha baada ya majukumu hayo kupewa Tito Vilanova tangu kuondoka kwa Pep Guardiola yamekwenda vyema.


"Namna tunavyofanya mazoezi ni mwendelezo ule ule na tunafanya kazi na watu wale wale, hatujaona tofauti yoyote," alisema.


"Tuko katika maandalizi ya msimu mpya hivyo unaweza kuona uchovu uliopo. Wanamiliki mpira vyema na kutufanya tukimbie sana lakini tutaongezeka ubora kwa kila mechi ijayo.


"Tunajituma kwa bidii mazoezini na ni lazima tuendelee hivyo ili kurejea katika kiwango chetu tayari kwa mechi muhimu."

No comments:

Post a Comment