Tuesday, July 31, 2012

KUMBE MBUNGE ANAYETAKA MAFISADI WAUAWE ANATISHA KWA BASTOLA


*NI MHE. ALI KESSY WA JIMBO LA NKASI KASKAZINI

Mhe. Ali Kessy
Mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia CCM, Mhe. Ali Mohamed Kessy, ameng’ara katika matumizi ya bastola na kuwaacha mbali washindani wake kadhaa, wakiwamo waheshimiwa Mathayo David, Martha Mlata na David Silinde.

Akizungumza bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alisema kuwa Kessy alionyesha umahiri mkubwa katika shindano la wabunge la kulenga shabaha kwa kutumia bastola lililofanyika mjini Dodoma na kuwapita akina Mathayo David na Martha Mlata.

Washindi wengine waliotangazwa bungeni jana katika shindano la kulenga shabaha ni pamoja na Waziri wa Ushirika na Masoko, Mhe. David, ambaye yeye aliibuka kidedea katika kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) huku Mhe. Mlata akishika nafasi ya pili katika kulenga shabaha kwa kutumia bunduki aina ya Light Machine Gun (LMG).     

Wakati Mhe. Ndugai akimtangaza Kessy kuwa ndiye mshindi katika kulenga shabaha kwa bastola, ukumbi mzima wa bunge uliripuka kwa shangwe na vicheko.

Haikufahamika mara moja ni kwanini wabunge walimshangilia sana Kessy, ingawa inaeleweka wazi kuwa mbunge huyo amekuwa maarufu sana kutokana na hoja yake anayoitoa kila mara ya kutaka watu wote wanaothibitika kujihusisha na vitendo vya ufisadi wasionewe huruma na sheria itungwe ya kutaka wauwawe kwa kunyongwa. 

Mhe. Kessy amekuwa akitetea hoja yake hiyo kwa maelezo kuwa vitendo vibaya vya kifisadi katika maeneo mbalimbali husababisha maafa ya watu wengi maskini wasiokuwa na hatia na hivyo, ni vizuri sasa nao wauawe kama inavyofanyika nchini China.

No comments:

Post a Comment