Tuesday, July 10, 2012

BARCELONA WAJA JUU MOURINHO KUFUTIWA ADHABU


Jose Mourinho
MADRID, Hispania
BARCELONA wamepinga vikali uamuzi wa Shirikisho la Soka la Hispania kufuta adhabu ya kifungo cha mechi mbili iliyokuwa ikimkabili kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho kwa kosa la kumtia kidole cha macho msimu uliopita aliyekuwa kocha msaidizi wa Barca, Tito Vilanova.

Ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa kabla ya kuanza kwa msimu wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania 2012-13 La Liga, tayari ‘bifu’ kali limeanza baina ya mahasimu hao wa jadi.

Msemaji wa Barca, Toni Freixa amesema kwamba msamaha aliopewa Mourinho, ikiwa ni sehemu ya misamaha ya jumla iliyotolewa kwa wachezaji na makocha, unaharibu picha ya soka la Hispania na pia unachochea zaidi kufanyika kwa vitendo vingine vya aina hiyo.

Mourinho alipewa adhabu ya kufungiwa baada ya kumtovuga Vilanova, ambaye sasa ndiye kocha wa Barcelona aliyerithi mikoba ya kocha aliyekataa kusaini mkataba mpya, Pep Guardiola. Vilanova pia amenufaika na msamaha huo kwani pia alikuwa akikabiliwa na adhabu ya kufungiwa mechi moja kwa kosa la kujibu mapigo ya Mourinho.

Freixa amesema kuwa rais wa Barca, Sandro Rosell ameelezea kutofurahishwa kwa klabu yao kufuatia msamaha alioupata Mourinho baada ya adhabu kuondolewa kwenye mkutano wa bodi ya shirikisho la soka uliofanyika jana mjini Madrid.

"Kadri tunavyoelewa, shambulizi dhidi ya kocha linastahili adhabu," Freixa alisema kupitia tovuti ya Barca (www.fcbarcelona.com).

"Uamuzi huu hauna maana kwamba mgomvi hana hatia, lakini unafanya waamini kwamba wanaweza kuendelea kushambulia watu wengine bila kuwa na hofu ya kuadhibiwa," aliongeza.

"Si mfano mzuri kwa soka la Hispania ikiwa kosa hili litapita bila ya kaudhibiwa."

No comments:

Post a Comment