Friday, June 29, 2012

SIMBA KUANZA NA URA, YANGA NA WARUNDI KAGAME, AZAM WAPEWA WAZENJI

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye (kulia) akizungumza na wanahabari katika Ofisi za TFF, mchana huu. Kushoto ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Na Prince Akbar
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame watafungua dimba na Atletico ya Burundi katika mchezo wa Kundi C wa michuano hiyo, Julai 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati wapinzani wao wa jadi Simba SC waliowekwa Kundi A, wataanza dhidi ya URA ya Uganda Julai 16, kwenye Uwanja huo huo.

Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano hiyo, Azam FC wao wataanza dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ya Kundi B kwenye Uwanja wa Chamazi Julai 15.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye amesema katika mkutano na wanahabari mchana huu kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam kuwa, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) itashiriki kama timu mualikwa.

Aidha, habari za kusikitisha ni kwamba, Musonye amesema Sudan, Ethiopia, Eritrea na Somalia hazitaleta wawakilishi wao kwa sababu mbalimbali.

Wakati Ethiopia ligi yao inaanza wiki hii, Sudan wawakilishi wao wapo kwenye michuano ya Afrika na wameshindwa kuteua timu mbadala. Somalia wawakilishi wao Elman wamebadilisha uongozi, hivyo bado hawajajipanga na Eritrea kutokana na desturi ya wachezaji wao kuzamia kila wanapokuja kwenye mashindano, wameondolewa.

“Wameondolewa kwa sababu mbili, kwanza nchi yao imeomba ipewe muda kulifanyia kazi sual hilo, na sisi pia (CECAFA) tunalitafutia ufumbuzi,” alisema Musonye.

Lakini Musonye amekiri kitendo cha kuyatoa mashindano hayo mwanzoni mwa mwaka hadi katikati ya mwaka kimechangia baadhi ya timu kutoshiriki na amesema tayari amewasilisha pendekezo kwenye Mkutano Mkuu ili mashindano yarejee kufanyika mwanzoni mwa mwaka kama ilivyokuwa awali.

Kundi A lina timu za Simba, URA ya Uganda, Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Ports ya Djibouti. Azam, Mafunzo ya Zanzibar na Tusker ya Kenya ziko kundi B.

Yanga inaunda kundi C lenye timu za APR ya Rwanda, Wau Salaam ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi.

Timu nane zitaingia robo fainali itakayochezwa Julai 23 na 24 mwaka huu. Kundi A na C kila moja litatoa timu tatu kwenda robo fainali wakati B litatoa timu mbili.

Kuhusu mechi ya ufunguzi ya Simba kuchezwa Julai 16, ambayo itakuwa Jumatatu badala ya Jumapili, Musonye alisema kwamba imetokana na kwamba Julai 15, Uwanja wa Taifa kutakuwa na fainali za Copa Coca Cola, ambayo maandalizi yake yote yamekamilika.

Yanga ndio mabingwa watetezi wa mashindano baada ya kuifunga Simba SC katika fainali mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Bingwa wa michuano hiyo atapata dola 30,000, makamu bingwa dola 20,000 na mshindi wa tatu dola 10,000. Michuano hiyo itaoneshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya SuperSport.

 
RATIBA KAMILI YA KOMBE LA KAGAME 2012
CHANZO: www.bongostaz.blogspot.com

No comments:

Post a Comment