Monday, December 24, 2012

MESSI AFUNGA MWAKA NA REKODI KIBAO

Lionel Messi

LIONEL Messi amemaliza mwaka 2012 kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo wakati akiuanza, ya kufunga. Amefunga jumla ya magoli 91, na kuipita kwa magoli 6 rekodi iliyodumu kwa miaka 40 ya magoli 85 iliyowekwa na gwiji wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Gerd 'Torpedo' Muller mwaka 1972.

Pamoja na hiyo, Messi a.k.a 'La Pulga' amekuwa mchezaji wa sita tu wa Barcelona katika historia ya klabu hiyo kufunga katika mechi saba mfululizo. Kufikia sasa, wachezaji pekee waliofanya hivyo ni Martín (mechi 10 mfululizo), Ronaldo (10), Cesar Rodriguez (7), Kubala (7) na Johan Cruyff (7). Messi sasa amejumuika katika orodha hiyo na anaweza kushika nafasi ya tatu miongoni mwao kama atafunga goli dhidi ya Espanyol katika mechi ya mahasimu wa Catalunya Januari 6.

Messi pia anaenda katika mapumziko ya Krismasi akiongoza kirahisi orodha ya wafungaji wa La Liga akiwa na mabao 25. Tayari ameshafunga nusu ya magoli aliyofunga msimu mzima uliopita ilhali ndiyo kwanza kuna mechi mbili bado za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa msimu huu.

La Pulga amemaliza mwaka kwa kuingia katika vitabu vya rekodi ambavyo huenda vikamshuhudia akishinda tuzo ya Ballon d’Or ya mwanasoka bora kwa mwaka wa nne mfululizo. Licha ya kutoshinda taji la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya wala la Ligi Kuu ya Hispania mwaka 2012, magoli yake aliyofunga yanampa nafasi kubwa zaidi ya kubeba tuzo hiyo kwa mara ya nne na kuwapiku magwiji kama Marco Van Basten au Michel Platini.

MASHABIKI REAL MADRID "WAMFUKUZA" MOURINHO... KURA YA MAONI YAPIGWA... ASILIMIA 82 WASEMA AONDOKE

Jose Mourinho

MASHABIKI wa Real Madrid wametoa maamuzi yao. Wanataka Mourinho afukuzwe Bernabeu. Matokeo mabovu katika msimu huu hadi sasa, yanayoambatana na mivutano inayoripotiwa baina ya Mreno huyo na baadhi ya wachezaji na vyombo vya habari, imewachosha, na sasa wamesema "INATOSHA".

Baada ya kumuweka benchi nahodha Iker Casillas katika mechi yao dhidi ya Malaga imekuwa ni moja ya mambo yaliyowachefua mashabiki. Kufuatia utafiti uliofanywa na tovuti ya nchini Hispania  ulioweka swali lililosema "Real Madrid imfukuze Mourinho?" watu takriban 100,000 wa Real walijibu ambapo asilimia 82.4 ilisema "NDIYO".

Inaonekana sasa mapenzi yaliyokuwapo baina ya kocha huyo Mreno na mashabiki wake yamekwisha, na mvunjiko ulionekana katika mechi ya Kombe la Mfalme dhidi ya Alcoyano, ambapo mashabiki wengi wa Real walimzomea na kumpigia miluzi kocha wao, huku wengine wakidiriki hata kuwazomea wenzao waliojaribu kumsapoti Mourinho uwanjani.

Zaidi, jambo hili linaweza kuonekana hata katika mitandao yote mikubwa ya kijamii, ambapo maoni ya kumsapoti yanapotea na kugeuka kuwa shutuma.

Kitendo cha kumtupa benchi mmoja wa magwiji wa Real Madrid - Iker Casillas - inaonekana ni kuanzisha vita dhidi ya mashabiki damu wa Madrid wanaojulikana kama 'Madridistas'.

Mourinho inawezekana kwamba ameamua ama hajaamua kuondoka mwisho wa msimu, lakini lililo wazi ni kwamba hata kama hajaamua 'kuruka nje ya boti', kuna watu wengi sana wanaotaka kuona akitimuliwa.

DISKO TOTO MARUFUKU KESHO KRISMASI

Kamanda Kova

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amepiga marufuku Disko Toto katika sikukuu ya Krismasi kesho.

Kamanda Kova amesema leo kwamba wameamua kuchukua hatua hiyo kwa lengo la kulinda usalama wa watoto.

Alisema pia kutakuwa na ulinzi wa askari wa miguu, pikipiki, Land Rover na farasi kwa ajili ya kuhakikisha watu wanasherehekea sikukuu hiyo kwa amani.

Hatua hiyo inafuatia matukio kadhaa ya watoto kufariki wakati wakiwa katika kumbi za Disko Toto.

Septemba 2010 watoto wawili walifariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya baada ya kukosa hewa ukumbini walikokuwa wamejazana kusherehekea Sikukuu ya Idd katika ukumbi wa disko wa Luxury Pub ulioko Temeke, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilifuatia jingine lililotokea Oktoba mosi mwaka 2008, wakati watoto 19 walipofariki dunia kwa kukosa hewa kwenye ukumbi wa Disco wa Bubbles unaomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Tabora.

FERGUSON ASIFU MCHANGO WA VAN PERSIE... MAGOLI YAKE YANGETOLEWA MAN UTD INGEKUWA INASHIKA NAFASI YA 8

Robin Van Persie wa Manchester United akikokota ngoma wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012. Timu hizo zilitoka 1-1.

Robin van Persie wa Manchester United akishangilia kufunga goli la ushindi dhidi ya Manchester City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Etihad Desemba 9, 2012. Man U walishinda 3-2.

Robin van Persie wa Manchester United akishangilia kufunga goli la ushindi dhidi ya Manchester City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Etihad Desemba 9, 2012. Man U walishinda 3-2.

KOCHA Alex Ferguson amesifu mchango mkubwa wa Robin van Persie klabuni Manchester United.

Magoli 12 katika mechi 18 kutoka kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 yameisaidia klabu yake mpya kwenda Krismasi ikiongoza ligi kuu ya England kwa tofauti ya pointi nne kileleni.

"Mimi huwa ni mgumu kutaja umuhimu wa mtu mmoja-mmoja kikosini. Lakini wakati mwingine unaona kwamba jambo hilo ni gumu," kocha huyo wa Man Utd alisema.

Man U ilipoteza ubingwa wa ligi msimu uliopita kutokana na tofauti ya magoli lakini kwa sasa wao ndiyo wanaoongoza kwa magoli mengi ya kufunga shukrani kwa Mholanzi huyo.

Mshindi huyo wa tuzo mbili za Mwanasoka Bora wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa na Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari, amekuwa na mchango mkubwa Old Trafford tangu ajiunge katika kipindi kilichopita cha usajili akitokea Arsenal kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24, akifunga magoli 15 katika michuano yote.

Magoli ya Van Persie kikosini yamekuwa muhimu kutokana na alivyoyafunga kwenye ligi ambapo amefunga goli la kuongoza katika mechi tani na amefunga goli la ushindi katika mechi tano, huku la kukumbukwa zaidi likiwa muhimu zaidi katika ushindi wa 3-2 ugenini dhidi ya mahasimu Manchester City.

Kama magoli yake yangetolewa kutoka katika jumla ya magoli ya klabu yake, vinara wa ligi Man United wangepungukiwa pointi 15 na wangekuwa wanashika nafasi ya nane katika msimamo.

Jumla ya mabao yake katika michuano yote yamewazidi washambuliaji wengine wote wa Man United, huku Danny Welbeck akiwa amepitwa magoli 14, Wayne Rooney amepitwa magoli saba na Javier Hernandez 'Chicharito' akimkaribia kwa kuwa na magoli tisa.

Mchango wa Van Persie umefananishwa na ule wa gwiji Mfaransa Eric Cantona wakati alipoiongoza Man United kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi katika miaka 26 licha ya ukweli kwamba wakati akiwasili kutokea Leeds Novemba 1992 timu ya Ferguson ilikuwa katikati ya msimamo.

Akizungumza katika maandalizi yamechi yao ya ligi itakayochezwa katika Boxing Day nyumbani dhidi ya Newcastle, Ferguson alisema: Tulifanya hivyo wakati tulipomleta Eric Cantona Old Trafford ambapo alithibitisha kuwa ni mchezaji sahihi katika klabu sahihi kwa wakati sahihi.

"Alikuwa chachu ya mafanikio na nguzo ya kuelekea kwenye ubingwa wetu.

"Si lazima kununua mchezaji kwa bei inayoweka rekodi. Cristiano Ronaldo hatukumnunua kwa bei iliyoweka rekodi lakini alileta tofauti wakati alipochanua nasi na kuwa mchezaji anayeaminika kwa watu wengi zaidi kwamba ndiye bora zaidi duniani."

KESHI 'HASTUSHWI' NA MADONGO YA ODEMWINGIE

Stephen Keshi

KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi amesema "hakuna chuki binafsi" katika maamuzi yake ya kumuacha Peter Odemwingie nje ya kikosi kitakachocheza fainali za Mataifa ya Afrika.

Mshambuliaji huyo wa West Brom aliongeza kwa hasira baada ya kuachwa nje ya kikosi cha awali cha wachezaji 32 kilichotangazwa Jumamosi.

Odemwingie aliichezea kwa mara ya mwisho Super Eagles katika mechi ya Februari iliyomalizika kwa sare ya 0-0 dhidi ya Rwanda katika kuwania kufuzu kwa fainali hizo.

Katika ujumbe wa hasira kwenye Twitter, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alisema ameachwa kwa sababu ana kawaida ya kuongea ya moyoni.

Lakini Keshi ameiambia BBC World Service leo kwamba hastushwi na jinsi Odemwingie alivyolipokea suala hilo.

"Sina hata akaunti ya Facebook au Twitter hivyo hainisumbui hata kidogo," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa zamani wa Nigeria.

"Hakuna chochote 'spesho' kuhusu jambo hili. Odemwingie ni mchezaji mzuri lakini kwa sasa simhitaji.

"Yeye ni mweledi na anapaswa kulikubali hilo.

"Nigeria imejaaliwa wachezaji wazuri wengi na hatuwezi kumuita kila mchezaji.

"Hatuko katika vita na yeyote, tunajaribu kufanya kazi yetu."

Odemwingie, ambaye aliichezea Nigeria kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2004, 2006, 2008 na 2010, alimtuhumu Keshi kumkosea heshima kwa kumtomtaarifu jambo hilo yeye binafsi.

"Kila kocha ana mipango yango na mbinu zake - kama sifai katika mipango yako, tafadhali kuwa muwazi niambie moja kwa moja," Odemwingie aliiambia BBC Sport.

"Kwa miaka 10 nimejitoa kwa moyo wangu wote kwa taifa langu uwanjani, nimecheza kwa ajili ya taifa na mashabiki, sio kwa mtu binafsi," alisema.

Odemwingie, ambaye alizaliwa nchini Uzbekistan ambako baba yake Mnigeria alikuwa ameweka maskani, alisema ameangaliwa vibaya na Keshi na shirikisho kwa sababu amekuwa akizungumza hali ya soka la Nigeria.

ODEMWINGIE ACHUKIA KUACHWA KIKOSI CHA NIGERIA KITAKACHOENDA AFCON AFRIKA KUSINI

Peter Osaze Odemwingie


PETER Odemwingie ameelezea kukerwa kwake na kitendo cha kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria kitakachoenda kucheza fainali za Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini mwezi ujao.

Mshambuliaji huyo wa West Bromwich Albion aliichezea Nigeria mara ya mwisho Februari katika sare ya 0-0 ya kuwania kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Rwanda.

"Kila kocha ana mipango na mbinu zake - kama sifai katika mipango yako, tafadhali kuwa muwazi niambie moja kwa moja," Odemwingie aliiambia BBC Sport.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 aliichezea Nigeria katika fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2004, 2006, 2008 na 2010.

"Kwa miaka 10 nimejitoa kwa moyo wangu wote kwa taifa langu uwanjani, nimecheza kwa ajili ya taifa na mashabiki, sio kwa mtu binafsi," alisema.

Odemwingie anaamini ameachwa kwa sababu mara kwa mara amekuwa akizungumza yaliyo moyoni mwake kuhusu timu ya taifa.

"Kwa sababu huwa ninazungumza mambo yanapokuwa si sawa, nadhani baadhi ya watu wanakosa amani ninapokuwa muwazi," alisema.

"Hakuna mtu anayepewa kipaumbele, wacheza soka ni kama watu wengine wa kawaida tu na si viumbe waliokamilika.

"Kuna historia ndefu ya matatizo baina ya wachezaji, makocha na shirikisho na hayajamalizwa - nchi inaendelea kuchechemea.

"Soka lina maana kubwa kwa Wanigeria na mashabiki wanastahili mafanikio na sio kulishwa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari."

Hata hivyo, Odemwingie amesema hatafunga milango ya kuichezea tena Nigeria kama ataitwa.

"Ni jambo la ghafla na hakika sijui, lakini watu binafsi wanabadilika ila matatizo yanabaki," Odemwingie alisema.

"Kama nafasi ya kuchezea nchi yangu itakuja tena, nitazungumza na baba yangu na wale walio karibu nami - kisha tutaona.

"Binafsi, natakiwa kucheza mara kwa mara kwenye klabu yangu na kuweka nguvu zangu katika kuwa mtu bora kila siku.

"Kwa sasa, ninachoweza kufanya ni kuitakia timu mafanikio nchini Afrika Kusini."

'Super Eagles' wanaanza kampeni zao za Mataifa ya Afrika dhidi ya Burkina Faso Januari 21 na kisha watawakabili mabingwa Zambia na baadaye Ethiopia katika Kundi C.

VAN PERSIE ANA BAHATI KUBAKI HAI - FERGIE

Robin Van Persie wa Manchester United akizikunja na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.
Robin Van Persie wa Manchester United akizikunja na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.

Robin Van Persie wa Manchester United akitenganishwa asizichape na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.

Robin Van Persie wa Manchester United akimlalamikia refa Michael Oliver kuhusu kitendo alichofanyiwa na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.
Robin Van Persie wa Manchester United akitenganishwa asizichape na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.

Refa Michael Oliver akiwapatanisha Robin Van Persie wa Manchester United na Ashley Williams wa Swansea City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012.
Ashley Williams wa Swansea City akiosha mpira uliompiga kisogoni Van Persie (chini kushoto) na kuzua ugomvi baina yao.

SIR Alex Ferguson amesema Robin van Persie "ana bahati kubaki hai" baada ya kupigwa na mpira kisogoni na Ashley Williams wa Swansea wakati wa mechi yao iliyoisha kwa sare ya 1-1.

Van Persie alikuwa amelala "sakafuni" wakati Williams 'alipoosha' mpira jirani yake huku refa akiwa tayari ameshapuliza firimbi ya kuashiria kuna madhambi yamefanyika.

Ferguson anaona kwamba Van Persie alikuwa na bahati sana kuepuka majeraha makubwa.

"Robin van Persie ana bahati kubaki hai. Kilikuwa ni kitendo kisicho cha kiungwana kutoka kwa mchezaji wao," Ferguson aliiambia BBC Sport.

Van Persie na Williams waliingia katika majibizano makali baada ya tukio hilo.

"Anapaswa kufungiwa na FA. Robin angeweza kuvunjika shingo."
Kocha wa huyo wa Man United alisema Williams (28) alidhamiria kumlenga na mpira Van Persie, ambaye alinyanyuka kwa hasira - na wachezaji wote wawili walilimwa njano na refa Michael Oliver.

Ferguson aliongeza kwenye Sky Sports: "Katika suala la Van Persie, uliona wazi kwamba angeweza kuuawa.

"Anapaswa kufungiwa muda mrefu kwa sababu lile ni jambo la hatari zaidi kwenye uwanja wa soka nililopata kuliona kwa miaka mingi.

"Lilikuwa ni tukio la makusudi. Firimbi ilikuwa imeshalia, mpira ulikuwa umesimamishwa na akafanya jambo lile mbele ya refa, angeweza kumuua kijana.

"Kilikuwa ni kitendo kisicho cha kiungwana kabisa, anapaswa kufungiwa kwa muda mrefu."

Williams alikanusha kumpiga Van Persie makusudi.

"Nimeona katika TV na hayo ni maoni yake [Ferguson]," alisema Williams.

"Kila mtu anakuwa na maoni yake lakini kwa mtazamo wangu, nilijaribu kuomba radhi uwanjani lakini mambo yakakuzwa.

"Niliubutua mpira kwa fadhaa na wala sikujaribu kumlenga kichwani.

"Naelewa kwanini amekasirika. Hata mimi ningekasirika kama mpira ungenipiga kwa kasi ile."

Mshambuliaji wa Man U, Wayne Rooney alijaribu kutuliza hali kuhusu tukio hilo.

"Nadhani ni moja ya matukio yale," alisema. "Firimbi ilikuwa imelia, beki alikuwa anajiandaa kuosha na ukampiga kisogoni. Nadhani yalikuwa maamuzi sahihi yaliyofanywa na refa."