Ashley Williams wa Swansea City akiosha mpira uliompiga kisogoni Van Persie (chini kushoto) na kuzua ugomvi baina yao. |
SIR Alex Ferguson amesema Robin van Persie "ana bahati kubaki hai" baada ya kupigwa na mpira kisogoni na Ashley Williams wa Swansea wakati wa mechi yao iliyoisha kwa sare ya 1-1.
Van Persie alikuwa amelala "sakafuni" wakati Williams 'alipoosha' mpira jirani yake huku refa akiwa tayari ameshapuliza firimbi ya kuashiria kuna madhambi yamefanyika.
Ferguson anaona kwamba Van Persie alikuwa na bahati sana kuepuka majeraha makubwa.
"Robin van Persie ana bahati kubaki hai. Kilikuwa ni kitendo kisicho cha kiungwana kutoka kwa mchezaji wao," Ferguson aliiambia BBC Sport.
Van Persie na Williams waliingia katika majibizano makali baada ya tukio hilo.
"Anapaswa kufungiwa na FA. Robin angeweza kuvunjika shingo."
Kocha wa huyo wa Man United alisema Williams (28) alidhamiria kumlenga na mpira Van Persie, ambaye alinyanyuka kwa hasira - na wachezaji wote wawili walilimwa njano na refa Michael Oliver.
Ferguson aliongeza kwenye Sky Sports: "Katika suala la Van Persie, uliona wazi kwamba angeweza kuuawa.
"Anapaswa kufungiwa muda mrefu kwa sababu lile ni jambo la hatari zaidi kwenye uwanja wa soka nililopata kuliona kwa miaka mingi.
"Lilikuwa ni tukio la makusudi. Firimbi ilikuwa imeshalia, mpira ulikuwa umesimamishwa na akafanya jambo lile mbele ya refa, angeweza kumuua kijana.
"Kilikuwa ni kitendo kisicho cha kiungwana kabisa, anapaswa kufungiwa kwa muda mrefu."
Williams alikanusha kumpiga Van Persie makusudi.
"Nimeona katika TV na hayo ni maoni yake [Ferguson]," alisema Williams.
"Kila mtu anakuwa na maoni yake lakini kwa mtazamo wangu, nilijaribu kuomba radhi uwanjani lakini mambo yakakuzwa.
"Niliubutua mpira kwa fadhaa na wala sikujaribu kumlenga kichwani.
"Naelewa kwanini amekasirika. Hata mimi ningekasirika kama mpira ungenipiga kwa kasi ile."
Mshambuliaji wa Man U, Wayne Rooney alijaribu kutuliza hali kuhusu tukio hilo.
"Nadhani ni moja ya matukio yale," alisema. "Firimbi ilikuwa imelia, beki alikuwa anajiandaa kuosha na ukampiga kisogoni. Nadhani yalikuwa maamuzi sahihi yaliyofanywa na refa."
No comments:
Post a Comment