Stephen Keshi |
KOCHA wa timu ya taifa ya Nigeria, Stephen Keshi amesema "hakuna chuki binafsi" katika maamuzi yake ya kumuacha Peter Odemwingie nje ya kikosi kitakachocheza fainali za Mataifa ya Afrika.
Mshambuliaji huyo wa West Brom aliongeza kwa hasira baada ya kuachwa nje ya kikosi cha awali cha wachezaji 32 kilichotangazwa Jumamosi.
Odemwingie aliichezea kwa mara ya mwisho Super Eagles katika mechi ya Februari iliyomalizika kwa sare ya 0-0 dhidi ya Rwanda katika kuwania kufuzu kwa fainali hizo.
Katika ujumbe wa hasira kwenye Twitter, nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 alisema ameachwa kwa sababu ana kawaida ya kuongea ya moyoni.
Lakini Keshi ameiambia BBC World Service leo kwamba hastushwi na jinsi Odemwingie alivyolipokea suala hilo.
"Sina hata akaunti ya Facebook au Twitter hivyo hainisumbui hata kidogo," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa zamani wa Nigeria.
"Hakuna chochote 'spesho' kuhusu jambo hili. Odemwingie ni mchezaji mzuri lakini kwa sasa simhitaji.
"Yeye ni mweledi na anapaswa kulikubali hilo.
"Nigeria imejaaliwa wachezaji wazuri wengi na hatuwezi kumuita kila mchezaji.
"Hatuko katika vita na yeyote, tunajaribu kufanya kazi yetu."
Odemwingie, ambaye aliichezea Nigeria kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2004, 2006, 2008 na 2010, alimtuhumu Keshi kumkosea heshima kwa kumtomtaarifu jambo hilo yeye binafsi.
"Kila kocha ana mipango yango na mbinu zake - kama sifai katika mipango yako, tafadhali kuwa muwazi niambie moja kwa moja," Odemwingie aliiambia BBC Sport.
"Kwa miaka 10 nimejitoa kwa moyo wangu wote kwa taifa langu uwanjani, nimecheza kwa ajili ya taifa na mashabiki, sio kwa mtu binafsi," alisema.
Odemwingie, ambaye alizaliwa nchini Uzbekistan ambako baba yake Mnigeria alikuwa ameweka maskani, alisema ameangaliwa vibaya na Keshi na shirikisho kwa sababu amekuwa akizungumza hali ya soka la Nigeria.
No comments:
Post a Comment