Peter Osaze Odemwingie |
PETER Odemwingie ameelezea kukerwa kwake na kitendo cha kuachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria kitakachoenda kucheza fainali za Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini mwezi ujao.
Mshambuliaji huyo wa West Bromwich Albion aliichezea Nigeria mara ya mwisho Februari katika sare ya 0-0 ya kuwania kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Rwanda.
"Kila kocha ana mipango na mbinu zake - kama sifai katika mipango yako, tafadhali kuwa muwazi niambie moja kwa moja," Odemwingie aliiambia BBC Sport.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 aliichezea Nigeria katika fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2004, 2006, 2008 na 2010.
"Kwa miaka 10 nimejitoa kwa moyo wangu wote kwa taifa langu uwanjani, nimecheza kwa ajili ya taifa na mashabiki, sio kwa mtu binafsi," alisema.
Odemwingie anaamini ameachwa kwa sababu mara kwa mara amekuwa akizungumza yaliyo moyoni mwake kuhusu timu ya taifa.
"Kwa sababu huwa ninazungumza mambo yanapokuwa si sawa, nadhani baadhi ya watu wanakosa amani ninapokuwa muwazi," alisema.
"Hakuna mtu anayepewa kipaumbele, wacheza soka ni kama watu wengine wa kawaida tu na si viumbe waliokamilika.
"Kuna historia ndefu ya matatizo baina ya wachezaji, makocha na shirikisho na hayajamalizwa - nchi inaendelea kuchechemea.
"Soka lina maana kubwa kwa Wanigeria na mashabiki wanastahili mafanikio na sio kulishwa taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari."
Hata hivyo, Odemwingie amesema hatafunga milango ya kuichezea tena Nigeria kama ataitwa.
"Ni jambo la ghafla na hakika sijui, lakini watu binafsi wanabadilika ila matatizo yanabaki," Odemwingie alisema.
"Kama nafasi ya kuchezea nchi yangu itakuja tena, nitazungumza na baba yangu na wale walio karibu nami - kisha tutaona.
"Binafsi, natakiwa kucheza mara kwa mara kwenye klabu yangu na kuweka nguvu zangu katika kuwa mtu bora kila siku.
"Kwa sasa, ninachoweza kufanya ni kuitakia timu mafanikio nchini Afrika Kusini."
'Super Eagles' wanaanza kampeni zao za Mataifa ya Afrika dhidi ya Burkina Faso Januari 21 na kisha watawakabili mabingwa Zambia na baadaye Ethiopia katika Kundi C.
No comments:
Post a Comment