Monday, December 24, 2012

FERGUSON ASIFU MCHANGO WA VAN PERSIE... MAGOLI YAKE YANGETOLEWA MAN UTD INGEKUWA INASHIKA NAFASI YA 8

Robin Van Persie wa Manchester United akikokota ngoma wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Swansea City kwenye Uwanja wa Liberty mjini Swansea nchini Wales jana Desemba 23, 2012. Timu hizo zilitoka 1-1.

Robin van Persie wa Manchester United akishangilia kufunga goli la ushindi dhidi ya Manchester City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Etihad Desemba 9, 2012. Man U walishinda 3-2.

Robin van Persie wa Manchester United akishangilia kufunga goli la ushindi dhidi ya Manchester City wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Etihad Desemba 9, 2012. Man U walishinda 3-2.

KOCHA Alex Ferguson amesifu mchango mkubwa wa Robin van Persie klabuni Manchester United.

Magoli 12 katika mechi 18 kutoka kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 yameisaidia klabu yake mpya kwenda Krismasi ikiongoza ligi kuu ya England kwa tofauti ya pointi nne kileleni.

"Mimi huwa ni mgumu kutaja umuhimu wa mtu mmoja-mmoja kikosini. Lakini wakati mwingine unaona kwamba jambo hilo ni gumu," kocha huyo wa Man Utd alisema.

Man U ilipoteza ubingwa wa ligi msimu uliopita kutokana na tofauti ya magoli lakini kwa sasa wao ndiyo wanaoongoza kwa magoli mengi ya kufunga shukrani kwa Mholanzi huyo.

Mshindi huyo wa tuzo mbili za Mwanasoka Bora wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa na Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari, amekuwa na mchango mkubwa Old Trafford tangu ajiunge katika kipindi kilichopita cha usajili akitokea Arsenal kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24, akifunga magoli 15 katika michuano yote.

Magoli ya Van Persie kikosini yamekuwa muhimu kutokana na alivyoyafunga kwenye ligi ambapo amefunga goli la kuongoza katika mechi tani na amefunga goli la ushindi katika mechi tano, huku la kukumbukwa zaidi likiwa muhimu zaidi katika ushindi wa 3-2 ugenini dhidi ya mahasimu Manchester City.

Kama magoli yake yangetolewa kutoka katika jumla ya magoli ya klabu yake, vinara wa ligi Man United wangepungukiwa pointi 15 na wangekuwa wanashika nafasi ya nane katika msimamo.

Jumla ya mabao yake katika michuano yote yamewazidi washambuliaji wengine wote wa Man United, huku Danny Welbeck akiwa amepitwa magoli 14, Wayne Rooney amepitwa magoli saba na Javier Hernandez 'Chicharito' akimkaribia kwa kuwa na magoli tisa.

Mchango wa Van Persie umefananishwa na ule wa gwiji Mfaransa Eric Cantona wakati alipoiongoza Man United kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi katika miaka 26 licha ya ukweli kwamba wakati akiwasili kutokea Leeds Novemba 1992 timu ya Ferguson ilikuwa katikati ya msimamo.

Akizungumza katika maandalizi yamechi yao ya ligi itakayochezwa katika Boxing Day nyumbani dhidi ya Newcastle, Ferguson alisema: Tulifanya hivyo wakati tulipomleta Eric Cantona Old Trafford ambapo alithibitisha kuwa ni mchezaji sahihi katika klabu sahihi kwa wakati sahihi.

"Alikuwa chachu ya mafanikio na nguzo ya kuelekea kwenye ubingwa wetu.

"Si lazima kununua mchezaji kwa bei inayoweka rekodi. Cristiano Ronaldo hatukumnunua kwa bei iliyoweka rekodi lakini alileta tofauti wakati alipochanua nasi na kuwa mchezaji anayeaminika kwa watu wengi zaidi kwamba ndiye bora zaidi duniani."

No comments:

Post a Comment