Saturday, September 22, 2012

VILANOVA: MESSI ATAWAFUNIKA KINA PELE, MARADONA

Lionel Messi
Tito Vilanova
BARCELONA, Hispania
Kocha wa Barcelona, Tito Vilanova amesema kwamba Lionel Messi anaelekea kuwa mwanasoka bora zaidi wa wakati wote duniani na amefichua kwamba kila mmoja ndani ya klabu yao anaamini kwamba atastaafu soka lake akiwa Barca.


Mfalme wa soka, Pele ndiye anayechukuliwa na wengi kuwa ni mwanasoka bora wa wakati wote duniani, akifuatiwa na Muargentina Diego Maradona,

Rais wa Barcelona, Sandro Rosell amethibitisha wiki hii kwamba klabu yake inapanga kumpa ofa ya mkataba mpya straika huyo wa kimataifa wa Argentina, licha ya kwamba mkataba wake wa sasa utamalizika 2016. Na kocha wa klabu hiyo, Vilanova amerudia tena kauli hiyo ya vigogo hao kutaka kuendelea kuwa na Messi kwa muda mrefu zaidi .

"Yeye ndiye Mwansoka Bora wa Dunia. Kama siyo tayari ameshakuwa mkali kuliko wote katika historia ya soka, atamaliza soka lake akiwa hivyo," kocha huyo mwenye miaka 44 amewaambia waandishi wa habari.
"Kwa wote ndani ya Barca, itakuwa furaha sana kuwa naye hapa katika kipindi chake chote cha uchezaji. Hamtamuona tena mchezaji mwingine kama Messi."

Mchezaji huyo wa zamani wa Celta pia alikanusha madai kwamba ameanza kuwazia mechi ijayo ya 'Clasico' dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Real Madrid itakayopigwa Oktoba 7, badala yake akisema kwamba mechi ya leo watakayocheza nyumbani dhidi ya Granada ndiyo pekee anayoiwazia.

"Sifikirii kuhusu Clasico," amesema kiungo huyo wa zamani wa kikosi B cha Barcelona.
"Ninachoangalia sasa ni kufikisha pointi 15 kutokana mechi tano tulizocheza kufikia mwisho wa wiki hii.

"Hilo halijafanyika mara nyingi katika historia. Kichwani mwangu nafikiria Granada tu, Granada na Granada. Ni kama nyie (waandishi wa habari) kuniuliza mimi kuhusu mechi dhidi ya Real Madrid ambayo ni ya raundi ya pili katika ratiba (baada ya mechi ya leo).

"Dhidi ya Granada, kinachotuongezea ari ni ushindi, sio kufikiria kwamba tutapaa kwa pointi 11 zaidi ya Real Madrid. Kwa vile hilo halituhusu, kulifikiria ni kupoteza muda. Nimeziona mechi za Granada na huwa wanajipanga vizuri na pia ni hatari sana kwa mashambulizi ya kustukiza."

Vilanova pia alikiri kutojua ni nani ampange katika nafasi ya beki wa kati katika mechi ya leo baada ya kukosekana kwa Carles Puyol na Gerard Pique ambao wote wanasumbuliwa na majeraha. Yosso mwenye kipaji, Marc Bartra anaweza kupata nafasi hiyo, wakati Alex Song pia akiwa na nafasi ya kucheza nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment