CHELSEA walicharuka kwa staili ya aina yake na kuisambaratisha kabisa Aston Villa iliyo katika kiwango cha juu na kurejea katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, huku vinara Manchester United wakishikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Swansea.
Fernando Torres aliendeleza kasi yake ya kufufua makali chini ya kocha wa Blues, Rafael Benitez kwa kufunga goli tamu la kichwa katika dakika ya tatu tu ya mchezo.
Na goli jingine zuri la 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni kutoka kwa David Luiz likafanya matokeo yawe 2-0 kabla ya kichwa cha Branislav Ivanovic kuwapeleka Chelsea mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 3-0. Torres sasa amefunga magoli 7 katika mechi 6 zilizopita chini ya kocha wake wa zamani aliyemfanya atishe klabuni Liverpool, Benitez.
Frank Lampard alisherehekea mechi yake ya 500 akiwa na Chelsea kwa kufunga goli la shuti la mbali katika dakika ya 60 na magoli mawili kutoka kwa Ramires, penalti ya Oscar na goli la juhudi binafsi kutoka kwa Eden Hazard yalikamilisha kipigo hicho cha mbwa-mwizi.
Pamoja na uthibitisho wa Chelsea kufufuka chini ya Benitez, kipigo hicho kiliweka rekodi za Ligi Kuu ya England.
Matokeo hayo yaliweka rekodi ya kuwa mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu ya England kwa wachezaji saba tofauti wa timu moja kufunga katika mechi moja na pia iliifikia rekodi ya Chelsea ya kushinda magoli mengi zaidi kama iliposhinda 8-0 dhidi ya Wigan Mei 2010.
Kikosi cha Villa ambacho hakikubadilishwa kilienda katika mechi hiyo kikiwa katika kiwango cha juu huku kikitokea kuishangaza Liverpool kwa kuichapa 3-1 Jumamosi iliyopita.
Kipigo hicho kimekuwa ndicho kikubwa zaidi kwa Aston Villa katika ligi kuu. Waliwahi kulala 7-0 mara tano huku kipigo cha karibu zaidi cha idadi hiyo ya mabao kikija mwaka 1950.
Manchester United wanaenda katika Sikukuu ya Krismasi wakiongoza kwa tofauti ya pointi 4 baada ya sare ya kufadhaisha ya 1-1 ugenini dhidi ya Swansea.
Kichwa cha Patrice Evra kiliwapa Man United goli la kuongoza kutokana na kocha ya Robin van Persie, lakini Swansea walijibu mapigo kupitia kwa kinara wa mabao Michu aliyefunga kiulaini baada ya shuti la Jonathan De Guzman kupanguliwa mbele yake na kipa David De Gea.
Man U waligongesha nguzo za goli mara mbili baada ya mapumziko, na Van Persie alicharuka kwa hasira wakati shuti la Ashley Williams lilipompiga kisogoni wakati akiwa amelala 'sakafuni'.
Williams aliosha mpira katika dakika ya 74 na ukampiga kisogoni Van Persie, ambaye alinyanyuka kutaka kumkunja beki huyo, na wote wakalimwa kadi za njano.
Van Persie alikaribia kuifungia timu yake goli la ushindi wakati shuti lake lilipogonga besela na mchezaji mwenzake Michael Carrick pia kichwa chake kiligonga nguzo ya lango.
Ilikuwa ni sare ya kwanza kwa Man United, ambao wameweza kutoruhusu goli mara nne tu msimu huu na ambao wamefungwa magoli 25, lakini safu yao kali ya ushambuliaji imekuwa ikiwaokoa.
Nafasi | Timu | Mechi | Goal Difference | Pointi |
---|---|---|---|---|
1 | Man Utd | 18 | 19 | 43 |
2 | Man City | 18 | 19 | 39 |
3 | Chelsea | 17 | 19 | 32 |
4 | Arsenal | 18 | 14 | 30 |
5 | Everton | 18 | 8 | 30 |
6 | Tottenham | 18 | 5 | 30 |
7 | West Brom | 18 | 4 | 30 |
8 | Liverpool | 18 | 4 | 25 |
9 | Stoke | 18 | 2 | 25 |
10 | Norwich | 18 | -7 | 25 |
11 | Swansea | 18 | 4 | 24 |
12 | West Ham | 18 | 0 | 23 |
13 | Fulham | 18 | -5 | 20 |
14 | Newcastle | 18 | -6 | 20 |
15 | Sunderland | 18 | -5 | 19 |
16 | Aston Villa | 18 | -17 | 18 |
17 | Southampton | 17 | -11 | 15 |
18 | Wigan | 18 | -15 | 15 |
19 | QPR | 18 | -16 | 10 |
20 | Reading | 18 | -16 | 9 |
No comments:
Post a Comment