Wednesday, October 3, 2012
UNHCR YAUNGA MKONO WAKIMBIZI WALIOKO TANZANIA KURUDI KWAO
Na Mwandishi Wetu, Geneva, Uswisi
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limeipongeza na kuihakikishia Tanzania kwamba linaunga mkono mpango wa Serikali hiyo kuwarejesha nyumbani wakimbizi kutoka Burundi walioko katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila na kuifunga rasmi kambi hiyo ifikapo mwezi Desemba 2012
Aidha Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeipongeza Tanzania kwa kwa jitihada zake za kuwahifadhi wakimbizi kutoka nchi za Maziwa Makuu na nchi mbalimbali duniani pamoja na kudumisha amani nchini humo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Geneva na Mkurugenzi Mkuu wa UNHCR, Antonio Gutteres wakati wa mkutano wa Kamati Tendaji(Executive Committee) ya shirika hilo uliofanyika Geneva Uswisi.
Mkurugenzi huyo wa UNHCR aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa UNHCR na jumuia ya kimataifa inaunga mkono mpango wa Serikali ya Tanzania kuwarejesha Burundi wakimbizi wa Kambi ya Mtabila na kuifunga Kambi hiyo ifikapo Desemba 31 mwaka huu.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt . Emmanuel Nchimbi alisema kuwa Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi 100,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi ambao wako nchini kutokana na vita vilivyokuwa nchini mwao.
Aliongeza kuwa katika kutafuta suluhisho la wakimbizi nchini, Serikali kwa kushirikiana na UNHCR mwaka uliopita iliendesha mahojiano katika Kambi ya Mtabila inayowahifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma ili kutaka kujua idadi ya wakimbizi wanaotaka kurejea nchini mwao kwa hiari.
Dkt. Nchimbi alisema kuwa mahojiano hayo yaliyozingatia Sheria ya Kimataifa ya wakimbizi na Sheria za Kimataifa inahusika masuala ya ubinadamu ambapo wakimbizi 2,400 waliomba kuendelea kupata hifadhi hapa nchini na hivyo kuhamishiwa kambi nyingine.
Aidha wakimbizi 38,050 walionyesha nia ya kurudi kwao kwa hiari na hivyo kupewa muda hadi Desemba 31 mwaka huu ili waweze kujiandaa kurejea katika nchi yao.
Kufuatia hali hiyo Waziri huyo alitoa wito kwa wadau kuungana na Tanzania katika kuhakikisha kuwa wakimbizi hao 38,050 wanarudishwa kwao ifikapo Desemba 31 mwaka huu.
Aidha kuhusu suala la wakiingia nchini mnamo mwaka 1972, Waziri huyo alisema kuwa bado suala lao linajadiliwa ili kuangalia kweli wapewe uraia wa Tanzania au wasipewe.
Mhe. Nchimbi aliwashukuru wadau mbalimbali kwa jitihada zao za kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na wakimbizi na kuahidi kuendelea kuwapokea wakimbizi watakaohitaji hifadhi nchini Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment