Sergio Ramos |
BEKI wa kimataifa wa Hispania, Sergio Ramos alionyesha kwamba hamuogopi hata chembe kocha wa klabu yake ya Real Madrid, Jose Mourinho baada ya kuvaa jezi mbili kwa wakati mmoja katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania dhidi ya Derpotivo Coruna kwa nia ya kumuumbua kocha huyo, imefahamika.
Beki huyo aliyeripotiwa kuwa na migogoro ya mara kwa mara na Mourinho, alivalia kwa ndani jezi ya kiungo Mesut Ozil katika kipindi cha pili na kusaka goli kwa udi na uvumba ili ashangilie mbele ya mashabiki wao kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu kwa nia ya kumuumbua kocha wao ambaye alimtoa nje kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani na kumuingiza Mbrazili Kaka.
Mourinho alimtoa Ozil wakati wa mapumziko baada ya kumbwatukia pembeni ya mstari wa uwanja katika kipindi cha kwanza. Kocha huyo Mreno aliendelea kumbwatukia Ozil wakati wa mapumziko na kumtoa nje kabla ya kumuingiza Kaka badala yake.
Ilionekana kwamba Ramos alitaka amuunge mkono Ozil kwa kuvaa jezi yake katika kipindi chote cha pili na kusaka goli maalum la kumzawadia.
Beki huyo wa kati, alionekana kila mara akidhamiria kufunga goli wakati wa kupigwa kwa mipira ya kutenga na pia kuingia ndani ya eneo la hatari la Derpotivo Coruna kila mara waliposhambulia.
Hata hivyo, beki huyo aliambulia patupu baada ya kushindwa kufunga goli na kuonyesha jezi ya Ozil kwa nia ya kuonyesha namna alivyokuwa akimuunga mkono baada ya kutolewa na Mourinho.
Ramos, aliyeachwa nje ya kikosi cha timu yake katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester City, amekuwa mara kadhaa akirushiana vijembe na Mourinho wakati wa mikutano na waandishi wa habari.
Baada ya kurejeshwa kikosini katika mechi yao dhidi ya Rayo Vallecano, beki huyo aliwaambia waandishi wa habari: "Sijui kama sikupangwa kwa sababu ya adhabu au ni kwa sababu za kiufundi. Jibu halipaswi kutolewa na mimi. Siku zote huwa sizungumzii hadharani mambo haya ya ndani."
No comments:
Post a Comment