LISBON, Ureno
BEKI wa kati wa Barcelona, Carles Puyol alipelekwa hospitalini baada ya kiwiko cha cha mkono wake wa kushoto kuhama kutoka mahala pake katika ushindi wao wa 2-0 wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Benfica jana usiku bna atakosa mechi ya 'El Clasico' dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Nou Camp Jumapili.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza baada ya kupona majeraha ya goti, alianguka vibaya wakati akiwania kufunga kwa mpira wa kona.
Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 34 alichukuliwa kwa machela akiugulia maumivu katika dakika ya 78 na nafasi yake kuchukuliwa na Alex Song wakati wachezaji wenzake wakiangalia kwa hofu.
"Tunasubi taarifa zaidi lakini atakosa 'Clasico'," kocha wa Barca, Tito Vilanova aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi hiyo.
Majeraha hayo yamekuja katika kipindi kigumu kwa Barcelona ambao beki mwenzake wa kati Gerard Pique pia ni mgonjwa.
Barca ilishinda mjini Lisbon, ushindi wao wa pili katika Kundi G, shukrani kwa magoli kutoka kwa Alexis Sanchez na Cesc Fabregas.
"Sasa ni lazima tusahau kuhusu Ligi ya Klabu Bingwa na tuwe na fursa ya kufanya vizuri katika mechi ya nyumbani Jumapili," alisema beki wa kulia wa Barca, Dani Alves, ambaye alionekana kuguswa sana na kuumia kwa Puyol. "Tunajua itakuwa mechi ngumu sana."
Barca wako pointi nane juu ya Real katika La Liga baada ya mechi sita.
No comments:
Post a Comment