Wednesday, October 3, 2012

SIMBA, YANGA NGUVU SAWA... YANGA WAMALIZA 10


Goooooooo!. Kipa wa Yanga, Yaw Berko akishindwa kuzuia shuti la Amri Kiemba (hayupo pichani) wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka 1-1. 
Mashabiki wa timu ya Simba wakishangilia wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka 1-1. 
Mashabiki wa timu ya Simba wakishangilia wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo. Timu hizo zilitoka 1-1. 

YANGA wameshindwa kulipa kisasi cha magoli 5-0 katika mechi ambayo walimaliza wakiwa 10 huku goli la penalti likiwapa sare ya 1-1 dhidi ya Simba katika mechi ya watani wa jadi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Simon Msuva alitolewa kwa kadi ya pili ya njano kwa Yanga lakini Haruna Moshi 'Boban' atajihesabu ni mwenye bahati kubaki uwanjani dakika chache tangu aingie kuchukua nafasi ya Jonas Mkude pale alipoonekana kumkanyaga kwenye goti beki wa Yanga, Kelvin Yondani, ambaye alibebwa kwa machela na hakurudi uwanjani kutokana na jeraha hilo. Mwamuzi  Mathew Akrama alimwonyesha kadi ya njano.

Magoli kutoka kwa Amri Kiemba wa Simba na penalti ya Said Bahanunzi wa Yanga ndiyo yaliyoamua matokeo ya mechi hiyo ambayo Yanga walikuwa wakijaribu kulipa kisasi cha kipigo cha magoli 5-0 walichopata katika mechi yao ya mwisho wa msimu uliopita.

Mbele ya mashabiki 59,000 kwa mujibu wa takwimu za kituo cha Supersport kilichorusha kwa mara ya kwanza leo mechi ya ligi kuu baina ya mahasimu hao, Simba walianza mechi vizuri zaidi na wakapata goli zuri la kuongoza katika dakika ya 4 tu kupitia kwa kiungo wa zamani wa Yanga, Amri Kiemba kufuatia krosi safi ya Mwinyi Kazimoto.

Simba waliendelea kutawala katika dakika za mwanzo na kufikisha asilimia 59 dhidi ya 41 za kumiliki mpira.

Katika muda huo, Wekundu wa Msimbazi walikuwa wakionana kwa pasi fupi fupi za haraka na walitawala eneo la kiungo na wangeweza kupata magoli zaidi.

Baadaye Yanga walionekana kutulia na kuanza kutawala "possession" huku kioo cha Supersport kikionyesha asilimia 69 kwa Yanga dhidi ya 31 za Simba.

Mbuyu Twite, ambaye alizigombanisha timu hizo mbili kwa kusaini Simba kabla ya kubadili msimamo na kujiunga na Yanga, alikaribia kuifungia Yanga goli la kusawazisha lakini bahati ilikuwa kwa Wekundu wa Msimbazi kwani shuti lake kali liligonga ‘besela’ na kurudi uwanjani katika dakika ya 31.  

Kocha mpya wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts, ambaye alikuwa akiiongoza klabu hiyo kwa mara ya kwanza leo, aligundua udhaifu katika dimba la kati lililokuwa likitawaliwa na viungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto, Kiemba na Jonas Mkude. Akamtoa mshambuliaji Hamis Kiiza ambaye alionekana kupwaya na akionekana ana maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Frank Domayo katika dakika ya 35, ambaye aliingia kujaza eneo la kati pamoja na Athumani Idd 'Chuji', Haruna Niyonzima na Nizar Khalfani.

Mabadiliko hayo yaliimarisha Yanga ikazidi kutawala katika eneo hilo na kumalizia kipindi cha kwanza ikiwa imecheza vizuri zaidi licha ya kuwa nyuma kwa goli 1-0.

Baada ya kuona ameshatawala kiungo na anahitaji nguvu zaidi ya kutafuta goli la kusawazisha, Brandts alianza kipindi cha pili kwa kumpumzisha kiungo Nizar Khalfani na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Didier Kavumbagu, mabadiliko yaliyoongeza mashambulizi.

Kiemba alikaribia kurudia kufunga goli kama la kipindi cha kwanza mapema katika kipindi cha pili wakati alipofumua shuti kali la umbali wa mita 25 ambalo hata hivyo lilidakwa kifundi na Yaw Berko.

Presha mfululizo ya Yanga ilizaa matunda wakati mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki, Said Bahanunzi alipofungua akaunti yake ya mabao katika ligi kuu kwa kufunga penalti iliyotolewa na mwamuzi Akrama baada ya beki wa Simba Paul Ngalema kushika mpira ndani ya boksi wakati akijaribu kuokoa kwa kichwa mpira wa kona katika dakika ya 65.

Bahanunzi ambaye alishutumiwa kwa kucheza chini ya kiwango tangu alipotengeneza jina kubwa katika Kombe la Kagame, alipiga penalti yake kwa shuti la katikati ya lango lililoenda kutinga kwenye dari la lango wakati Kaseja akiruka chini kushoto.

Baada ya goli hilo, Yanga walionekana kutawala mchezo huku Kaseja akiwa shujaa kwa kuokoa mashuti mengi na hawakupungua makali hata Msuva alipotolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi beki Juma Nyosso.

Mrisho Ngassa, aliyecheza kwa mara ya kwanza mechi ya watani wa jadi akiwa amevaa jezi nyekundu alionekana tishio katika matukio kadhaa na wachezaji wa timu yake ya zamani walihitaji kumpa ulinzi wa zaidi ya mtu mmoja kila aliposhika mpira.

Baadhi ya mashabiki wa Simba walionekana wakitoka uwanjani mapema pengine kwa kutoridhishwa na kiwango cha timu yao ilivyocheza dhidi ya wachezaji 10 wa Yanga.

Hata hivyo, sare ilitosha kuiimarisha Simba kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 13 baada ya mechi 5 huku Yanga ikifikisha pointi 8.

Kabla ya mechi hiyo, timu za vijana za U-20 za timu hizo zilitoka sare ya magoli 2-2, huku Simba ikikomboa yote baada ya kutanguliwa kwa magoli 2-0.

Vikosi vilikuwa:

Yanga:
Yaw Berko, Mbuyu Twite, Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani/ Juma Abdul (dk.81), Athuman Iddi ‘Chuji’, Nizar Halfan/ Didier Kavumbagu (dk.46), Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Said Bahanunzi, Hamis Kiiza/ Frank Domayo (dk.35) na Simon Msuva.

Simba:
Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Cholo’, Paul Ngalema, Juma Nyoso, Shomari Kapombe, Jonas Mkude/ Haruna Moshi ‘Boban’ (dk.68), Amir Kiemba, Mwinyi Kazimoto/ Ramadhani Chombo ‘Redondo’ (dk.87), Felix Sunzu, Edward Christopher/ Daniel Akuffor (dk.64) na Mrisho Ngassa.

No comments:

Post a Comment