Carles Puyol wa Barcelona (kushoto) na Lima wa Benfica wakiwania mpira wa kichwa wakati wa mechi yao ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Luz mjini Lisbon, jana Oktoba 2, 2012. (Picha: REUTERS) |
LISBON, Ureno
Beki wa kati wa Barcelona, Carles Puyol alikimbiziwa hospitali baada ya kutengua kiwiko cha mkono wake wa kushoto katika ushindi wao wa ugenini wa 2-0 kwenye mechi ya Kundi G la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Benfica jana na hivyo atakosa mechi ya 'El Clasico' watakayocheza Jumapili dhidi ya Real Madrid kwenye Uwanja wa Nou Camp.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, akicheza katika mechi yake ya kwanza tangu apone jeraha la goti, aliangukia mkono aliporuka kuufuata mpira wa kona.
Nahodha huyo wa Barca mwenye miaka 34 alitolewa katika machela huku akionekana kuwa na maumivu makali katika dakika ya 78 na nafasi yake ikachukuliwa na Alex Song wakati wenzake wakionekana kustushwa na tukio hilo.
"Tunasubiri taarifa zaidi lakini ni wazi kwamba atakosa mechi ya 'Clasico'," kocha wa Barca, Tito Vilanova aliwaambia waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.
Jeraha limekuja katika wakati mgumu kwa Barcelona ambayo pia inamkosa pacha wa Puyol katika nafasi ya ulinzi wa kati, Gerard Pique ambaye pia ni majeruhi.
Barca ilishinda mjini Lisbon, ukiwa ni ushindi wao wa pili katika mechi zao mbili za Kundi G, shukrani zikiwaendea wafungaji Alexis Sanchez na Cesc Fabregas.
"Sasa tunapaswa kusahahu kuhusu Ligi ya Klabu Bingwa na kuangalia namna ya kuitumia vyema fursa ya kufanya vizuri tukiwa nyumbani (Jumapili)," alisema beki wa pembeni wa Barca, Dani Alves, ambaye alionekana kustushwa na jeraha alilopata Puyol.
"Tunajua itakuwa mechi ngumu."
Barcelona wako kileleni mwa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa pointi nane zaidi ya mahasimu wao wa jadi, Real Madrid ikiwa ni baada ya kila timu kucheza mechi sita.
No comments:
Post a Comment