Thursday, October 4, 2012

MUUZA MAGAZETI ALIYEDAIWA KUUAWA MAANDAMANO YA CHADEMA MOROGORO HUYU HAPA... AELEZA ALIVYONUSURIKA..!


Sijafa jamani... muuza magazeti Kassim Mdangu aliyedhaniwa ni Ali Zona aliyeuawa Agosti 27 wakati wa maandamano ya Chadema mkoani Morogoro. (Picha: Sanula Athanas)

Kassim Mdangu (Picha: Sanula Athanas)

Kassim Mdangu akimhudumia mteja (Picha: Sanula Athanas)


Muuza magazeti, Kasim Mdangu akionyesha alama za damu ya marehemu Ali Zona maeneo Msamvu, Mbuyuni mkoani Morogoro Septemba 19, 2012. (Picha: Sanula Athanas)
Kasim Mdangu akiongea na mwandishi wa habari hii, Sanula Athanas katika eneo lake la biasdhara. (Picha: Sanula Athanas)
Ni saa 10:09 alfajiri: Kasim Mdangu anapokea magazeti kwenye kituo cha magazeti mjini Morogoro Septemba 20, 2012. (Picha: Sanula Athanas)
Na Sanula Athanas
MUUZA magazeti aliyedaiwa kuuawa wakati wa maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA maeneo ya Msamvu mjini Morogoro Agosti 27 mwaka huu, Kassim Mdangu ameeleza namna alivyonusurika katika tukio hilo lililoua mtu mmoja na wengine kujeruhiwa.

Akiongea na mwandishi wa habari hii katika eneo analouzia magazeti yake mtaa wa Msamvu kata ya Mbuyuni, mjijini Morogoro Jumatano ya mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga (Septemba 19), Mdangu alikanusha taarifa hizo na kusema kwamba aliyeuawa ni mbeba mizigo, Ali Zona.

“Watu wengi walishangaa baada ya kuniona kwa sababu walipata taarifa kuwa nimeuawa wakati wa maandamano ya CHADEMA… ukweli ni kwamba aliyeuawa ni ‘kuli’ (mbeba mizigo) Ali,” alisema Mdangu.

Aliendelea kueleza kuwa Ali alikuwa akiishi mtaa wa Modeko ambao uko jirani na mtaa wao wa Msamvu na alikuwa akifanya kazi katika kituo cha magari ya mizigo yanayotoka mkoani Iringa kilichopo takriban mita 25 kutoka anapouzia magazeti.

Alisema kuwa wakati wafuasi wa CHADEMA wakikimbizana na polisi, yeye alikuwa kwenye ofisi yake hiyo akiuza magazeti na baadaye marehemu (Ali) alifika kununua maji mahali hapo.

“Marehemu alikuja kununua maji maana kipindi hicho tulikuwa tukiuza maji pia. Gari la Polisi lilifika hapa likasimama, polisi wakaanza kutuhoji ni kwanini tumefanya mkusanyiko wakati kulikuwa kumeshatolewa amri ya kutofanya maandamano... tukawaambia sisi hatukuwa na nia ya kuandamana. Wakaondoka,” alisema Mdangu.

“Baada ya kuondoka baadhi ya watu waliokuwa hapa wakaanza kuwazomea… kwa jinsi lile gari la Polisi lilivyogeuka, nilijua kabisa kwamba kinachofuata ni kichapo nikaamua kurtimua mbio. Marehemu hakukimbia maana tulimwacha hapa akipitia magazeti.

Ghafla tukasikia mlio kama wa risasi hivi, tuliporudi tukamkuta Ali ameanguka chini huku mwili wake ‘ukidundadunda’ na kichwa chake kilikuwa kimeharibika vibaya.”

Mdangu alisema kuwa alishangaa kuona vyombo vya habari vikiripoti kuwa aliyefariki katika tukio hilo ni muuza magazeti katika eneo ambalo anauzia (yeye) huku baadhi ya watu wakishtuka na wengine wanapokuwtana naye kupiga kelele na kumkimbia kwa sababu walipata taarifa kuwa ameuawa.

“Jambo hili limekuwa likinikosesha raha, lakini kaka yangu Mohamed amekuwa akinifariji na kunisihi niachane nalo kwa sababu mimi si wa kwanza kuzushiwa kifo,” alisema Mdangu.

Agosti 27 mwaka huu kuriripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini kuwa muuza magazeti Ali Zona aliuawa wakati wa Jeshi la Polisi likipambana na wafuasi wa CHADEMA ambao walikuwa wamejikusanya kwenda kwenye mkutano wa chama chao.

Hata hivyo, ripoti ya uchunguzi wa jeshi hilo kwa kushirikiana na madaktari, ilieleza kuwa kifo cha Ali kilisababishwa na kugongwa na kitu kizito kichwani.



No comments:

Post a Comment