Thursday, October 4, 2012

MECHI YA SIMBA v YANGA YAINGIZA SH. MIL 390, KLABU ZAAMBULIA MILIONI 93/-, MAKATO MAKUBWA YAZIDI KUZIUMIZA TIMU

Kiungo wa Simba, Amri Kiemba (katikati) akipongezwa na wachezaji wenzake kutoka kushoto Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Uhuru Selemani wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Timu hizo zilitoka 1-1.

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya watani wa jadi Yanga na Simba iliyochezwa jana (Oktoba 3 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 imeingiza Sh. 390,568,000, lakini makato makubwa kupitiliza katika uwanja huo yameendelea kutozinufaisha klabu.
 

Katika mgawo, Yanga na Simba kila moja zimepata Sh.milioni 93 ambazo jumla yake inakuwa ni Sh. milioni 186 wakati makato ni mengi zaidi kiasi ambacho klabu hizo mbili zinapata. Jumla ya makato ni Sh. milioni 203. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, watazamaji 50,455 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa 1 usiku kwa viingilio vya Sh. 5,000, Sh. 7,000, Sh. 10,000, Sh. 15,000, Sh. 20,000 na Sh. 30,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa Sh. 93,345,549.15 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni Sh. 59,578,169.49.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 240,000, kamishna wa mechi sh. 250,000, waamuzi sh. 591,000, mwamuzi wa akiba (reserve referee) sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.

Umeme sh. 750,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 5,860,000 wakati tiketi ni sh. 7,327,000. Gharama za mchezo sh. 31,115,183.05, uwanja sh. 31,115,183.05, Kamati ya Ligi sh. 31,115,183.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,669,109.83 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 12,446,073.22.

Wakati huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex na kushuhudiwa na washabiki tisa kwa kiingilio cha sh. 3,000 imeingiza sh. 27,000.

Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa VAT sh. 4,118.6 wakati kila timu ilipata sh. 6,864.3. Uwanja sh. 2,288.1, gharama za mchezo sh. 2,288.1, Kamati ya Ligi sh. 2,288.1, FDF sh. 1,372.8 na DRFA sh. 915.2

Katika mechi hiyo, kiungo Amri Kiemba aliifungia Simba goli lao katika dakika 4 kufuatia krosi ya Mwinyi Kazimoto kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa straika Said Bahanunzi katika dakika ya 65 kwa penalti iliyotolewa na Mathew Akrama baada ya 
beki wa Simba, Paul Ngalema kushika mpira ndani ya 18 wakati akijaribu kuokoa mpira wa kona kwa kichwa.

No comments:

Post a Comment