Ronaldo |
Dah... nini tena? |
CRISTIANO
Ronaldo anataka Real Madrid kumpa mkataba mpya utakaomuingizia paundi za
England milioni 25 (Sh. bilioni 62) kwa mwaka.
Straika
huyo ambaye hivi sasa hana furaha tena klabuni hapo ana “usongo” wa kutaka
kuanza mazungumzo mapya yatakayomfanya asaini mkataba wa kuichezea klabu hiyo
kwa miaka sita, licha ya kwamba hivi sasa bado amebakiza miaka mitatu kumaliza
mkataba wake.
Ronaldo,
27, analipwa mshahara wa paundi za England milioni 9.6 (Sh. bilioni 24) kwa
mwaka, lakini kutokana na mabadiliko ya sheria za kodi za Hispania, sasa kiasi
cha mshahara anaokwenda nao nyumbani baada ya makato kimepungua na kufikia
paundi za England milioni 7.2. (Sh. bilioni 18)
Hivi
sasa anataka alipwe mshahara utakaomfanya aende nyumbani kwake na paundi za
England milioni 12 (Sh. bilioni 30) kwa mwaka. Kwa madai yake hayo mapya, hata
kwa sheria ya awali ya kodi, itamaanisha kwamba sasa straika huyo alipwe malipo
ghafi (ya kabla ya kodi) kiasi cha paundi za England milioni 14.5 (Sh. bilioni
36) kwa mwaka.
Tatizo
la Real Madrid kwa sasa ni kwamba, ndani ya miaka miwili, kiwango cha kodi
atakacholipa Ronaldo kitapanda kutoka asilimia 24 hadi 52.
Na
hilo linamaanisha kwamba ili (Ronaldo) alipwe kiasi anachotaka baada ya kukatwa
kodi cha paundi za England milioni 12 (Sh. bilioni 30) kwa mwaka, mshahara wake
wa jumla kabla ya kodi unapaswa kuwa takriban paundi za England milioni 25 (Sh.
bilioni 62) kwa mwaka, sawa na paundi za England 480,000 (Sh. bilioni 1.2) kwa
wiki!
Ronaldo
amekuwa akitaka asainishwe mkataba mpya tangu Januari.
Hata
hivyo, wakuu wa Real Madrid wamekuwa wakipinga kiwango anachotaka na pande hizo
zimekuwa katika mazungumzo, hasa ikifahamika wazi kwamba kanuni mpya
inayozibana klabu juu ya ukomo wa matumizi ya fedha ya UEFA ikitarajiwa kuanza
kutumika miaka miwili ijayo.
Ronaldo
bado hajawasilisha maombi rasmi ya kutaka aongezewe mshahara, lakini wapambe
wake wanaamini kuwa anastahili kupewa mkataba mnono kuliko wa mwanasoka yeyote
duniani na kuipiku mikataba iliyosainiwa na mastraika Didier Drogba na Nicolas
Anelka wanaochezea klabu za Shenhua Shanghai nchini China.
Hadi
sasa ameshafunga mabao 150 katika mechi 149 za michuano yote tangu ajiunge na
klabu hiyo akitokea Manchester United miaka mitatu iliyopita, huku pia akiwa na
rekodi ya kushangaza ya kufunga mabao 114 katika mechi 104 za La Liga, Ligi Kuu
ya Hispania alizochezea klabu hiyo iliyomnunua kwa paundi za England milioni 80
(Sh. bilioni 197).
Na
bado pia thamani yake hailipiki kulinganisha na “mihela” anayoiingizia klabu ya
Real Madrid kupitia mauzo ya bidhaa mbalimbali na udhamini.
Straika
huyo nyota wa kimataifa wa Ureno ana kipengele ghali cha kuvunja mkataba wake
cha paundi za England milioni 791 (Sh. trilioni 2) lakini kwa kufichua kwamba
hana furaha baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wao wa Jumapili wa
mabao 3-0 dhidi ya Granada, amefungua milango ya uwezekano wa kuhama katika dirisha
lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Hata
hivyo, kumuuza Ronaldo bado kunaonekana kuwa ni uamuzi usiopewa nafasi kwa
sasa, lakini linaweza kutokea.
Katika
hatua nyingine, imeelezwa kuwa uhusiano wa Ronaldo na baadhi ya wachezaji
wenzake katika chumba cha kuvalia pia hautabiriki.
Inadaiwa
kwamba kuna msuguano kati ya wachezaji wanaozungumza Kireno — Ronaldo, Pepe,
Marcelo, Fabio Coentrao — na wanaozungumza
Kihispaniola, hasa nahodha Iker Casillas na Sergio Ramos.
Alipozungumza
na waandishi baada ya mechi dhidi ya Granada, Ronaldo alisema: “Sina furaha na
watu wa ndani ya klabu wanajua kuhusiana na hili. Hii ndiyo sababu kwanini sishangilii.
Ni suala la kikazi. Siwezi kulizungumzia zaidi.”
No comments:
Post a Comment