Kiungo wa Newcastle United, Hatem Ben Arfa akifunga goli dhidi ya Aston Villa wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England mjini Newcastle, kaskazini mwa England Septemba 2, 2012. Picha: REUTERS |
LONDON, England
ROBIN van Persie alifunga magoli mawili ya dakika za lala-salama na kukamilisha 'hat-trick' yake iliyowapa Manchester United ushindi wa aina yake wa 3-2 dhidi ya Southampton katika mechi yao ya Ligi Kuu ya England leo.
Mholanzi huyo alikosa penalti wakati timu yake ikiwa nyuma 2-1 na kuonekana kama Man U ilikuwa ikielekea katika kipigo chao cha pili katika mechi tatu za ufunguzi za ligi lakini alirekebisha makosa yake kwa magoli mawili katika dakika za lala salama na kuzoa pointi zote.
Goli lake la kichwa katika dakika ya 92 lilikuwa ni bao lake la 100 katika Ligi Kuu ya England na la nne katika mechi tatu alizoichezea Man U tangu alipojiunga akitokea Arsenal kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 24 katika kipindi cha usajili kilichomalizika Ijumaa.
Mapema leo, Lukas Podolski, mtu ambaye ana jukumu la kuziba pengo la Mholanzi huyo kwa Arsenal, alifungua akaunti yake ya mabao katika Ligi Kuu ya England katika ushindi wa 2-0 ugenini dhidi ya Liverpool. Goli jingine la Arsenal lilifungwa na Santi Cazorla.
Ulikuwa ni ushindi wa kwanza wa Arsenal, na magoli yao ya kwanza msimu huu, baada ya sare mbili za 0-0, wakati Liverpool pointi moja waliyonayo katika mechi zao tatu za kwanza za msimu inaweka rekodi ya mwanzo mbovu zaidi katika miaka 50.
Katika mechi nyingine ya leo jioni, Newcastle United walishikiliwa kwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Aston Villa, na kuwaacha Southampton wakiwa timu pekee ya Ligi Kuu ya England ambayo haijapata pointi hata moja.
No comments:
Post a Comment