Sunday, September 2, 2012

MBWANA SAMATTA AIDUNGUA TENA AL AHLY LEO NA KUPELEKA TP MAZEMBE NUSU FAINALI KLABU BINGWA AFRIKA ... SASA AFIKISHA MAGOLI SITA NA KUSHIKA NAFASI YA PILI KWA MABAO SAWA NA ABOUTRIKA, TRESOR MPUTU

Sherif Ekramy wa Al Ahly akisikitika baada ya kutunguliwa na Mbwana Samatta wa TP Mazembe wakati wa mechi yao ya Kundi B la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika leo.
Tunatishaaaa...! Samatta (kushoto) akiwa na mchezaji mwenzake wa TP Mazembe, Cheibane Traore.

Chinja chinja hao Al Ahly...! Mashabiki wa TP Mazembe wakiishangilia timu yao.
LUBUMBASHI, DR-Congo
MABAO kutoka kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na jingine la Deo Kanda yaliisaidia TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutinga nusu fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kushinda nyumbani 2-0 katika mechi yao ya Kundi B dhidi ya Al Ahly ya Misri mjini Lubumbashi leo.

Samatta na Kanda walifunga magoli yote katika kipindi cha pili na kuwapa pointi tatu zilizowaweka kileleni mwa kundi lao baada ya kufikisha pointi 10, wakifuatiwa na Al Ahly wenye pointi 10 pia lakini wakiwazidi kwa tofauti ya mabao.

Timu hizo zote zimejihakikishia kufuzu kutoka katika kundi lao baada ya kuiacha kwa pointi tano  Berekum Chelsea ya Ghana iliyoshikiliwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Zamalek katika mechi yao iliyochezwa leo pia huku kila timu ikiwa imebakiza mechi moja kukamilisha mechi zao.  Zamalek ya Misri iko mkiani mwa msimamo wa Kundi B baada ya kuambulia pointi moja tu na kuchapwa katika mechi zao nyingine zote.

Licha ya kurejea uwanjani kwa beki wao Wael Gomaa, Ahly walihaha kukabiliana na mashambulizi makali ya kina Samatta. Wageni walimudu mashambulizi ya Mazembe hadi mapumziko, lakini wakajikuta wakichemsha katika kipindi cha pili.

Mashambulizi mfululizo yaliwalipa Mazembe katika dakika ya 49 wakati Tresor Mputu alipomzunguka Gomaa upande wa kushoto kabla ya kutoa krosi iliyompita kipa wa Ahly, Sherif Ekramy kabla Samatta hajauwahi mpira huo na kuukwamisha wavuni.

Kanda aliwahakikishia ushindi Mazembe baada ya kuwafungia bao la pili katika dakika ya 61 kutokana na shuti kali la chini, akimalizia kazi kubwa iliyotokana na juhudi binafsi za Mputu, ambaye kuna wakati alikuwa akichungwa vikali na mabeki wa Ahly.

Baada ya kufunga bao hilo, Kanda alitolewa dakika sita baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Mtanzania Thomas Ulimwengu.

Kutokana na bao alilofunga leo, Samatta sasa amefikisha mabao sita na hivyo kuwafikia Mputu na Mohamed Aboutrika wa Al Ahly, wote wakikamata nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji wanaoongoza katika michuano hiyo huku kinara akiwa mshambuliaji wa Chelsea, Emmanuel Clottey ambaye hadi sasa ana mabao 12. 


Samatta pia amejiwekea rekodi ya aina yake msimu huu baada ya kuzinyanyasa klabu vigogo za Misri za Zamalek na Ahly, akizifunga kila moja katika mechi zao zote za nyumbani na ugenini.


Ahly watalazimika kuwafunga mahasimu wao wa jiji la Cairo, Zamalek na kuombea Mazembe washikiliwe na Chelsea katika mechi zao za mwisho ili wapande kileleni mwa msimamo wa kundi hilo kwani mabingwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wana faida ya kuwa na mabao mengi yaliyotokana na mechi zilizowakutanisha baina yao. Katika mechi yao iliyochezwa Cairo, Ahly walishinda 2-1.

Timu itakayomaliza katika nafasi ya pili itakumbana na kibarua kigumu cha kucheza dhidi ya Esperance ya Tunisia.

No comments:

Post a Comment