Sunday, September 2, 2012
AKUFFOR AZIDI KUNG'AA, MABEKI WAPYA WAZIDI KUJIFUNGA SIMBA... BOCCO MOTO ULE ULE, AWAPIGA MBILI COASTAL
STRAIKA mpya wa Simba, Daniel Akuffor, ameendeleza makali yake ya "kutupia" baada ya kufunga goli lililoipa timu yake sare ya 1-1 na kufuta makosa ya kujifunga yaliyofanywa na beki mpya kutoka Mali, Komalbil Keita, katika mechi yao ya kirafiki waliyomaliza wakiwa 10 dhidi ya Sony Sugar ya Kenya kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha leo.
Keita amejifunga kama ilivyotokea kwa beki mwingine mpya, Pascal Ochieng, aliyejiunga na Simba baada ya kukosa namba katika timu ya AFC ya Kenya, ambaye alijidungua wiki iliyopita katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mathare United, ambapo Simba ilishinda 2-1, magoli ya Wekundu wa Msimbazi yakifungwa na Akuffor na Mrisho Ngassa.
Akuffor alifunga goli hilo katika dakika ya 60 kufuatia piga nikupige langoni mwa timu ya Sony Sugar.
Keita alijifunga katika dakika ya 42 wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Samwel Onyango na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa nyuma 1-0.
Simba ilirejea kipindi cha pili ikiwa imewapumzisha Nasoro Said Masoud 'Chollo' na Salim Kinje na nafasi zao kuchukuliwa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Shomari Kapombe.
Simba walijikuta wakibaki 10 uwanjani baada ya mwamuzi Judith Gamba kumtoa kwa kadi nyekundu Uhuru Selemani kutokana na kumchezea rafu mbaya Vicent Ugufu wa Sony Sugar.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic alisema kuwa ubovu wa uwanja uliathiri timu yake lakini mechi walizocheza zimesaidia kuimarisha kikosi chake.
Alisema kwamba timu yake itarejea jijini Dar es Salaam Jumanne kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Septemba 11.
Aidha, katika mechi nyingine ya kirafiki iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, wenyeji Azam waliendelea na maandalizi mazuri ya kuwakabili Simba katika mechi yao ya Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa magoli 2-0.
Straika John Bocco aliyerejea kutoka Afrika Kusini alikoshindwa majaribio ya kujiunga na klabu ya Super Sport United ya huko, alifunga magoli yote mawili na kuwa amefunga magoli manne katika mechi mbili za kirafiki tangu aliporejea nchini. Wiki iliyopita, alifunga magoli yote mawili tena wakati Azam iliposhinda 2-0 dhidi ya African Lyon.
Kiwango cha juu cha Bocco kinatarajiwa kuwa tishio tena dhidi ya Simba katika mechi yao hiyo, baada ya straika huyo kuifunga Simba 'hat-trick' na kuitoa katika hatua ya robo fainali ya Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) 2012 katika kipigo cha 3-1 kwenye uwanja huo huo wa Taifa.
Kikosi cha Simba katika mechi ya Arusha kilikuwa; Juma Kaseja, Nasoro Masoud ‘Cholo’/Shomari Kapombe, Amir Maftah, Pascal Ochieng, Komalbil Keita, Mwinyi Kazimoto, Salim Kinje/Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Haruna Moshi ‘Boban’, Abdallah Juma/Edward Christopher, Daniel Akuffor na Mrisho Ngassa/Kigi Makasi.
Labels:
Michezo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment