Straika Radamel Falcao akiwa kazini. |
STRAIKA wa Atletico Madrid, Radamel Falcao amesisitiza kwamba hana mpango wa kuihama klabu yake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kuibuka uvumi unaomhusisha na mahasimu wao wa jiji, klabu ya Real Madrid.
Ilielezwa jana kwamba Manchester City na Chelsea zote zinatarajia kumsajili nyota huyo wa kimataifa wa Colombia, ambaye ana kipengele katika mkataba wake kinachomruhusu kuondoka kwa dau la euro milioni 60 (Sh. bilioni 125), wakati dirisha la kipindi cha usajili wa Januari litakapofunguliwa.
Lakini Falcao ameingilia kati na kusisitiza kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba msimamo wake uko palepale katika kucheza kwa uwezo wake wote kwa ajili ya klabu yake ya Atletico Madrid na timu ya taifa lake.
"Kila mmoja atambue wazi, ndoto zangu ni kuendelea kushinda mataji nikiwa na Atletico Madrid na kuisaidia Colombia kupat6a nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014," alisisitiza kupitia ukurasa wake huo wa mtandao wa kijamii.
Uvumi kuhusiana na kuondoka kwake ulipata nguvu zaidi wakati baba yake alipodai kwamba Falcao amejiweka tayari kwa uhamisho wa kwenda kujiunga na klabu iliyo na upinzani wa jadi katika jiji la Madrid ya Real Madrid.
"Ndoto yake ni kuona kwamba siku moja anaichezea Real Madrid," baba yake Falcao aitwaye Radamel Garcia alisema katika mahojiano yake katika kipindi cha redio cha El Gran Debate de Todelar nchini Colombia.
"Siku zote, tangu akiwa mdogo, amekuwa akitamani kuchezea klabu ile."
Garcia pia alikaririwa akikiri kwamba, kama uhamisho wa Falcao kwenda Real Madrid hautazaa matunda, Ligi Kuu ya England ndiyo itakayokuwa chaguo lake.
"Klabu nyingine za soka kama Manchester City na Chelsea zimekuwa zikivutiwa naye. Kama hatakwenda Real Madrid, basi atakwenda katika klabu za Ligi Kuu ya England," alisema.
Baba huyo wa Falcao aliendelea kusema kwamba haamini kama mwanawe atabaki Atletico Madrid kwa muda mrefu.
"Zaidi ya yote, anataka kwenda Real Madrid. Atahama timu yake mwisho wa msimu huu," alisema Garcia, akiongeza kwamba hajui kama mtoto wake atauzwa ama la, kabla ya ushindi wa Atletico Madrid katika mechi yao ya kuwania taji la Super Cup la Ulaya dhidi ya Chelsea.
No comments:
Post a Comment