Thursday, September 6, 2012

WIZARA YAKANUSHA WAZIRI NCHIMBI KUUNDA TUME KUHUSIANA NA TUKIO LA MAUAJI YA MWANDISHI DAUDI MWANGOSI WA CHANNEL TEN... YASEMA ALICHOUNDA WAZIRI NI KAMATI NA WALA SIO TUME.. NI SIKU MOJA TU BAADA YA TUNDU LISSU KUIITA KAMATI HIYO KUWA NI "KAMATI YA KIRAFIKI... KAMATI YA KITCHEN PARTY"

Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani.
"Hii tume ni danganya toto. Ni tume ya kitchen party, pengine... ni tume ya marafiki, kujadiliana namna ya kuondoa hivi vichwa vya habari vibaya, na hizi picha mbaya, za jeshi la polisi likiua mtu hadharani" -- Tundu Lissu akitoa mfano wa picha za magazeti zinazoonyesha namna Mwangosi alivyouawa. Hapa ni wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CHADEMA, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. 
Wizara ya Mambo ya Ndani imekanusha taarifa kuwa waziri wake Dk. Emmanuel Nchimbi ameunda Tume ya Uchunguzi kuhusiana na tukio lililosababaisha mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.

Katika taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na kusainiwa na msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga, imeelezwa kuwa alichofanya Waziri Nchimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari juzi Septemba 4 ilikuwa ni kutangaza "kamati" aliyounda kuhusiana na vurugu zilizotokea Septemba 2 katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa; ambapo katika vurugu hizo, mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi alipoteza maisha.



Taarifa hiyo imetolewa leo ikiwa ni baada ya siku moja tu tangu Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kusema chama chake hakiungi mkono "tume" hiyo na kuiita kuwa ni "Kamati ya Kitchen Party".




HII NDIO NAKALA YA TAARIFA YA LEO WIZARA YA MAMBO YA NDANI




SOMA TAARIFA YA TUNDU LISSU ALIYOTOA JANA WAKATI AKIPINGA "TUME" YA WAZIRI NCHIMBI NA KUIITA KUWA NI "KAMATI YA KITCHEN PARTY"

Naomba nianze kwanza kwa kuwapa pole ndugu waandishi wa habari, na wote ambao mko katika kazi hii kubwa ya uandishi wa habari kwa msiba mkubwa ambao, umewapateni kwa kuuliwa mwenzenu, marehemu David Mwangosi.


Kwavile, Mwangosi ameuawa, kwavile tangu jana tunaambiwa kuna tume imeundwa kuchunguza mauaji ya Mwangosi... na vilevile kwa sababu moja ya magazeti yanayoheshimika hapa nchini, leo limehoji kwenye kichwa cha mbele cha habari kwamba, HII TUME, INAWEZA IKAFANYA HAKI? Nazungumzia banner headline ya kwenye gazeti la The Guardian la leo...kwa hiyo naomba kwenye mkutano huu na waandishi wa habari, tuzungumzie hii tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya ndani, Dk. Nchimbi... na tuone ni kitu gani kinaendelea hapo.

Na naomba nianze kwa kusema kwamba, kwa sababu mbalimbali ambazo tutazieleza hapa... eeh, hii tume iliyoundwa kuchunguza mauaji ya mwandishi mwenzenu wa habari David Mwangosi,  ni tume ya marafiki, pengine yenye lengo, sio la kuchunguza mauaji ya Mwangosi, bali kurekebisha kidogo mahusiano kati ya serikali na vyombo vya habari.

Kwa hiyo si tume ya kuchunguza mauaji, ni tume ya kurekebisha mambo, ku-repair hii public relations disaster, ya iliyotokea, tarehe 2, juzi. ... ya  jeshi la polisi kukamatwa mchana kweupe, likiua mwandishi wa habari. Kwahiyo ni tume ambayo lengo lake, sio kuchunguza mauaji, lengo lake, ni kuondoa hii picha ya mauaji yaliyofanywa na jeshi la polisi hadharani, kwenye vichwa vya mbele vya magazeti. Hivyo ndivyo tunavyoiangalia sisi.

Na kwa sababu siyo tume ya kuchunguza mauaji. Na kwa sababu sio tume ya kuchunguza mauaji, sisi kama chama, hatutaiunga mkono. Tutawashauri wananchi wa Tanzania, wawe wanachama wetu wasiwe wanachama wetu, wasiiunge mkono, kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, ndugu waandishi wa habari, nani wanaounda tume ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria za nchi hii. Sheria za nchi hii, sheria ninayoizungumzia hapa inaitwa, Sheria ya Tume  za Uchunguzi. Ni ya mwaka 1962, ni sura ya 29 nadhani  ya sheria za Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi, tume za uchunguzi huwa zinaundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Tume za Uchunguzi zinapewa hadidu za rejea na rais.

Na tume za uchunguzi za namna hiyo, zinatoa ripoti kwa rais, au zinaweza zikatoa taarifa hadharani, ripoti yao hadharani endapo rais ataelekeza hivyo katika hadidu za rejea atakazowapa. Kwa hiyo masuala ya kuunda tume za uchunguzi, kwa mambo makubwa yanayotokea kitaifa, ni jukumu kisheria la rais, sio jukumu la waziri ambaye, anaowasimamia, ndio watuhumiwa wa hicho kinachotakiwa kichunguzwe.

Kwahiyo katika upeo huo, upeo wa kisheria... Waziri Nchimbi hana mamlaka yoyote kisheria, ya kuunda tume  ya kuchunguza mauaji yaliyofanywa dhidi ya David Mwangosi, na Jeshi la Polisi analolisimamia... hilo ni jambo la kwanza.

Jambo la pili, lina uhusiano kidogo na hili  la kwanza. Walioua ni Jeshi la Polisi. Sasa, inawezekana, polisi wameamuriwa waue, na wakubwa zao katika jeshi, au wakubwa zao kisiasa.  Wakubwa wa jeshi kisiasa, jeshi la polisi... mamlaka ya kisiasa ni Waziri. Na mkubwa wao wa juu kabisa, ni IGP katika mamlaka ya kiutendaji.

Sasa kama utachunguza mauaji, yaliyotokea waziwazi, unaweza, inawezekana, haya mauaji yaliyofanywa, yamefanywa kwa sababu ya amri za wanasiasa, au... wanasiasa kwa maana ya mamlaka ya kisiasa inayosimamia jeshi la polisi, Waziri Nchimbi. Au inawezekana, mauaji yameamuriwa na mkuu wa jeshi, au maafisa wengine wa jeshi wa juu.

Sasa hii tume inayoundwa na Waziri, yenye wateule wa Waziri,  ina uwezezo wa kumhoji Waziri?... kuona kama anahusika au hahusiki? Je, tume ambayo mmoja wa wajumbe wake ni kamishna wa Polisi Isaya Mngulu, inaweza ikamuita IGP Mwema? IGP anaweza akaamuriwa na wale wa chini yake, akina Mngulu, kwenda kutoa ushahidi mbele ya tume hiyo? Kiutendaji, haiwezekani.

Ndio maana waliotunga sheria ya tume za uchunguzi walisema, mamlaka ya kuunda tume za uchunguzi ni mamlaka ya rais. Kwa sababu, tume ikiundwa kwa mamlaka hayo, inakuwa ina-act kwa jina la rais. Inakuwa inafanya wajibu wake, kutokana na mamlaka ya rais. Kwa hiyo ukiitwa hata na Mngulu, wewe kama IGP au kama Waziri, unaitwa kwa sababu wanaokuita wamepata mamlaka ya rais.

Kwa sababu hizi mbili, hii tume ni danganya toto. Ni tume ya kitchen party, pengine... ni tume ya marafiki, kujadiliana namna ya kuondoa hivi vichwa vya habari vibaya, na hizi picha mbaya, za jeshi la polisi likiua mtu hadharani.

Lakini ndugu waandishi wa habari, kuna sababu zingine. Nani anayeongoza tume hii?
Jaji Steven Ihema... sasa kama mmekuwa mnafuatilia taarifa za hivi karibuni, Jaji Steven Ihema ametajwa, na aliyemtaja ni mimi mwenyewe... ametajwa kama mmoja wa majaji, ambao waliteuliwa, na kufanya kazi ya ujaji kinyume cha katiba... kinyume cha katiba. Aliteuliwa kuwa jaji enzi za Mkapa. Wakati wa Mkapa.

Ilipofika mwaka 2003, Jaji Steven Ihema, kwa sababu hakuwa anajua sheria, hajui kazi ya ujaji, alisharundika zaidi ya kesi 300, ambazo anashindwa kuziandikia hukumu, anashindwa kuzifanyia maamuzi kama jaji. Kwa hiyo ni mtu ambaye anajulikana kwa kutokuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya kisheria.

Na ndugu zangu naomba nirudie hili kwa sababu wanaweza kusema tumeanza maneno yetu.  Mwaka 2003, kabla mimi sijawa mbunge, kuna mtu anaitwa Joram Alute... Joram Alute ni mwenyekiti wa leo wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Singida... kwa sababu ya ubovu wa Jaji Ihema, Joram Alute alimuandikia Rais Mkapa wakati huo, barua, ya kumuomba, kumuondoa Jaji Ihema mahakama kuu kwa sababu Jaji Ihema hakuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya ujaji.

Miaka karibu 10 iliyopita, wana CCM, Joram Alute si mwanachama wa Chadema... ni mwenyekiti wa CCM wa mkoa na kwa sababu hiyo ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, aliwahi kumuandikia rais na kumwambia huyu mtu (Jaji Ihema) hafai kuwa jaji, either ni mvivu, au hajui namna ya kuandika hukumu, either way...hafai kuwa jaji.

Mwaka 2005, Jaji Ihema akawa amemaliza mkataba wa kwanza, akapewa mkataba wa pili wa kazi ya ujaji. Sasa, kwa msiojua, majaji wa nchi hii, ni tenured judges, majaji wanateuliwa kwa kwa mujibu wa katiba, majaji hawaajiriwi kwa mkataba. Sasa Ihema alipewa mkataba.

Na kwa sababu ya Ihema kupewa mkataba, kuna jaji mmoja wa mahakama kuu wakati huo, anaitwa Benard Luanda... Benard Luanda leo ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Benard Luanda, mwaka 2005, baada ya kuandikiwa na Jaji Manento... wakati huo ni Jaji Kiongozi, alikuwa Manento au Msumi...! Manento...! Kwamba Jaji Ihema amepewa mkataba mwingine, Jaji Benard Luanda aliandaa, aliandika waraka, uliosambazwa kwa majaji wote wa Mahakama Kuu, ambao alisema kwamba;  huyu Jaji Ihema si jaji kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kwa sababu katiba ya Tanzania hairuhusu majaji wa mkataba... majaji wanaoweza kuondolewa baada ya miezi mitatu, endapo waliowapa mkataba wataamua. Kwa hiyo ndani ya mahakama yenyewe, inajulikana Jaji Ihema ni mtu awa aina gani.

Leo, Jaji Ihema, baada ya kushindwa kazi ya ujaji, alipelekwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Tume ambayo imekuwa, ni tume ya kuficha uchafu wa viongozi wa umma. Sio tume ya kuangalia maadili yao, ni tume ya kuficha madhambi yao. Tume ambayo, imenyamaza miaka yote wakati viongozi wa umma wakishiriki katika kufilisi taifa letu. Leo huyu ndio mwenyekiti wa tume ya kuchunguza mauaji ya mwandishi wa habari. Swali... mtu wa aina hii, hawezi akafanya kazi kwa sababu hana uwezo kama ambavyo nimeelezea. Na vilevile, maadili yake ni ya mashaka. Hafai kuchunguza mauaji ya aina hii

Polisi Isaya Mngulu,  anaweza akamuita IGP Said Mwema kwenda kumhoji? Kama amri ya kuua ilitoka kwa IGP Mwema?... anaweza kumwita Waziri Nchimbi kama alitoa amri kwamba, Jeshi la Polisi washughulikieni CHADEMA, wakifanya mikutano ua? Kama walivyoua Arusha, kama walivyoua Morogoro juzi ... na hii ya mauaji ya Iringa  juzi kuamkia jana.

Hawa wengine waliobaki. Tunaambiwa kuna mtu ni mtaalam wa milipuko. Kanali.. Wapwe sijui...unaenda kuchunguza kitu gani? Mtu amepigwa, ukiangalia picha za magazeti, na picha ambazo zimesambaa kwenye mtandao... zilizotoka wakati huohuo, silaha iliyotumika inajulikana, ni ya kurushia maguruneti yale ya moshi... hata magazeti ya leo. Angalia hapa ... kwenye Tanzania Daima, na magazeti ya jana... silaha iliyotumika kumuua marehemu Mwangosi inafahamika, ni bomu la machozi, lililolengwa kwa mtu pointblank. Ndio maana lilimchanachana vile. Unaenda kuchunguza huko ili ujue kitu gani ambacho tayari hakijulikani.

Muuaji anajulikana, walioshirikiana naye wanajulikana, silaha ya mauaji inajulikana, marehemu anajulikana... unaita huyo mtaalam wa explosives, kama ni kweli mtaalam wa milipuko, ili akachunguze mlipuko upi ambao haujulikani.

Hawa wengine, Theophil Makunga, Pili Mtambalike, na nani mwingine? Ni waandishi wa habari. Ni waandishi wenzenu wa habari. Swali rahisi hapa ni je, Theophil Makunga na Pili Mtamablike, wana utaalam wa kufanya murder inquiring?

Wana utaalam wa kuchunguza vifo? Hii tume, ni tume ya marafiki, yenye lengo la kukosha mauaji yaliyofanywa na marafiki. Kwa vyovyote vile. Kwa vyovyote vile, hii si tume halali ya kuchunguza mauaji.

Lakini ndugu waandishi wa habari, kuna mengine ninayotaka niyazungumzie kidogo. Hadidu za rejea. Chanzo cha kifo. Hadidu ya wachunguze chanzo cha kifo. Je, nani miongoni mwenu ambaye hajui chanzo cha kifo cha marehemu David Mwangosi. Nani ambaye hajui kuwa ameuawa na askari? Ambaye hajaona hizo picha, hajasoma magazeti, hajaangalia televisheni siku ya tukio na baada ya tukio? Nani asiyejua chanzo cha kifo cha marehemu David Mwangosi? Kama chanzo kinajulikana, sisi tusiokuwa wataalam, wanakwenda kuchunguza, chanzo kipi kingine? Na nimesema muaaji anajulikana, hiyo silaha inajulikana, walioumizwa wanajulikana na wengine ni mapolisi... wanakwenda kuchunguza chanzo kipi cha mauaji kisichojulikana?

Anasema huyu bwana, uhusiano kati ya polisi na vyombo vya habari. Sasa tunachunguza mauaji au tunachunguza, kwanini polisi wanalumbana na waandishi wa habari. Hiyo ni mbili.

Tunaambiwa wanatakiwa wachunguze, nguvu iliyotumika ilikuwa kubwa kupita kiasi? Reasonably force... sasa, suala la nguvu ilikuwa kubwa au si kubwa, ni suala la kisheria. Kwa sababu gani, sheria zetu zinasema, kama umevamiwa na mtu, anataka kukuumiza, au anataka kumuumiza ndugu yako, au mwanao, au mtu unayemhusu, ukimdhibiti, ikatokea umemuua, si umeua? Kisheria hiyo ni reasonabe force. Hiyo ni nini? Ni reasonable force. Kwa hiyo issue ya reasonableness ya nguvu iliyotumika, ni suala la kisheria. Na ni suala la ushahidi vilevile. Mazingira yalikuwaje? Hizi taarifa za vyombo vya habari, na picha zake zinaonyesha huyu bwana alishakamatwa. Alikuwa amedhibitiwa, ameangushwa, halafu wakati huohuo, amenyooshewa hiyo bunduki ya kurusha mabomu. Yuko chini. Ukiangalia gazeti la Tanzania Daima la leo, yuko chini ameshikana na askari. Huyu mtu alishadhibitiwa. Alishafanya nini? Kama kweli alikuwa anafanya fujo, alikuwa ameshadhibitiwa. Sasa hilo suala la reasonable force, kama nguvu iliyotumika ni ya kiasi au la, sio suala la uchunguzi kwa sababu inajulikana huyu mtu ameuawa akiwa chini, ameshikilia kamera...ameshikilia kamera. Kifaa chake cha kazi. Tunakwenda kuchunguza kipi ambacho hakijulikani?

Sasa... tunaambiwa kazi nyingine ni kuchunguza mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa. Vyama vipi vya siasa? Mimi sijawahi kusikia jeshi la polisi limevunja maandamano ya CCM, au mikutano ya kisiasa ya CCM? Au mikutano inayoendelea sasa hivi Bububu? Sijawahi kusikia. Sasa, kwenda kuchunguza uhusiano wa Jeshi la Polisi sio na vyama vya kisiasa. Inakwenda kuchunguza uhusiano wa Jeshi la Polisi na Chadema.

Chadema ndio mikutano yetu imekuwa, either inashambuliwa na Jeshi la Polisi na watu kuuawa, au inapigwa marufuku na Jeshi la Polisi. Ndivyo ilivyokuwa Arusha Januari mwaka jana, ndivyo ambavyo ilikuwa Morogoro wiki iliyopita, ndivyo ilivyokuwa juzi kuachia jana Iringa. Sasa kama unataka kuchunguza mashusiano ya Jeshi la Polisi na Chadema, kwa mfano, kwanini Mngulu wa polisi yupo kwenye hiyo tume? Kwanini watu wa Chadema hawapo? Kwanini msajili wa vyama vya siasa au mjumbe kutoka ofisi ya msajili, hawapo?

Unachunguza mahusiano ya polisi na vyama vya siasa au unataka kutengeneza ripoto itakayosema Chadema walikosea, Jeshi la Polisi lilikuwa halali, walikuwa sawasawa tu kufanya walichofanya... hii sio tume ya uchunguzi, hii ni tume ya kufunika mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi. Sasa, nimesema kwa sababu gani... kwa sababu hizo, hatuwezi kukubaliana na hiyo tume ya Nchimbi.

Tunataka nini? Moja... moja... tunadhani kwamba kweli kuna haja ya kuchunguza matukio haya. Lakini sio matukio ya Iringa juzi kuamkia jana peke yake. Wiki iliyopita, Polisi wameua mwananchi Morogoro. Ali Zola... wamempiga risasi kichwani katika maandamano ya Chadema yaliyovunjwa na Jeshi la Polisi. Mwaka jana, Jeshi la Polisi limeua watu watatu kwenye maandamano ya Chadema Arusha. Maandamano yalikuwa ya amani mpaka yaliposhambuliwa na risasi za Jeshi la Polisi.

Mwaka jana huohuo, kuna mwanachama wa Chadema, ameuawa Igunga kwenye Uchaguzi Mdogo wa Igunga. Mwaka huu, mwezi wa nne, wa tatu wa nne, mwanachama wa Chadema, kiongozi wa Chadema Arumeru Mashariki, ameuawa kwa kuchinjwa baada ya uchaguzi mdogo.

Wiki iliyopita, mwananchi ameuawa na Jeshi la Polisi Morogoro. Juzi wameua mwandishi wa habari Iringa. Matukio yote haya, matukio yote haya, mpaka tunavyozungumza, hajayachunguzwa inavyostahili. Yakitokea Polis wanaunda tume, halafu mambo yanaisha. Hatutaki mambo haya yaishe. Kwahiyo tunachotaka, tunachodai, badala ya hii Tume ya marafiki wa Nchimbi, tunataka iundwe a Judicial Commission of Inquiry... Tume ya Uchunguzi ya Kijaji, itakayoongozwa na majaji wanaofahamika kwa uadilifu wao, sio hawa majaji wa kuokoteza wa Kikwete.

Majaji wanaofahamika kwa utendaji wao wa kazi, kwa uadilifu wao, kwa kutokuwa na doa katika uteuzi wao. Majaji... kama  itapendeza, wawe majaji ambao watakuwa ni wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, au wakichanganywa na wa Mahakama Kuu, ambao hawana mawaa, ambao si makanjanja. Ifanye uchunguzi wa wazi. Uchunguzi wa wazi waandishi wa habari, ina maana ni uchunguzi ambao utafanyika hadharani, mashahidi wataitwa na tume, watatoa ushahidi wao hadharani, watahojiwa na mawakili wa tume hadharani, watahojiwa na mawakili wa familia za wote hawa ambao wameathirika hadharani... na ripoti ikatoka hadharani.

Tume za aina hii kwetu zimekuwa hazipo. Lakini kwa mujibu wa sheria ya tume za uchunguzi, rais anaweza akaianzisha, na akaipa hiyo mandate na hadidu za rejea za kuchunguza haya mambo hadharani. Hatutaki tume  za uchunguzi za kificho kwa sababu uchunguzi wa kificho utatuletea majibu polisi hawakukosea, kama ambavyo wamesema juzi Morogoro. Wenyewe mtakumbuka mwaka jana, mimi mwenyewe nilipigwa na kuchaniwa nguo Tarime kwa sababu Polisi waliua tena, wakasema watafanya uchunguzi, mpaka leo hatujui.

Tunataka Judicial Commisssion of Inquiry ya aina hiyo niliyoisema, itakayofanya kazi kwa namna ambayo nimeipendekeza. Na tume ya aina hiyo, itakuwa na mamlaka ya kumuita mtu yeyote yule isipokuwa rais... kwa mujibu wa sheria ya tume za uchunguzi, rais hawezi akawa subject ya investigation au akaitwa kujieleza mbele ya tume, hiyo ndiyo sheria... we are prepared to consider on that. Tumejiandaa kwa hilo, lakini mtu mwingine yeyote, Nchimbi, mapolisi, IGP na maafande wake wote, wanaweza kuitwa mbele ya hiyo tume, wakajieleza na kuhojiwa hadharani, ukweli ukaanikwa hadharani. Nje ya hapo, hatuko tayari kuunga mkono hiki kinachoendelea, hii danganya toto inayoendelea.

Pili, kuna mambo tunataka yafanyike haraka iwezekanavyo kwa sababu tayari yanajulikana. Nimesema, muuaji anajulikana, silaha iliyotumika kwa mauaji inajulikana, walioshirkiana na muuaji wanajulijkana, aliyeuliwa anajulikana, walioumizwa wanajulikana, waliovunjiwa mkutano wao wanajulikana...kwa sababu hiyo, angalau inajulikana waliotenda makosa ni kina nani.

Tunadai, tunataka, hao maaskari wote, waliokuwepo katika tukio la hiyo, hayom matukio ya Iringa eneo la  Nyololo, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka ya mauaji. Nafahamu, nafahamu, nafahamu kwamba sio wote waliofyatua hiyo bunduki, hiyo rocket launch...sio wote. Lakini wanasheria wanafahamu. Kwenye sheria zetu za jinai, kuna kitu kinaitwa commona intention...lengo la pamoja. Mnapoenda kuiba, genge la wezi, kwa nia ya kwenda kuiba, wakati mnatekeleza hiyo commona intention, mmoja wenu akaua, wote mnahesabiwa ni wauaji. Hili genge la mapolisi, wakiongozwa na RPC Kamuhanda walikuwa na common intention. Mmoja wao ameua ... wote kisheria wameua. Wote wanatakiwa wakamatwe na kufunguliwa kesi ya mauaji, hilo ni jambo la kwanza na hilo ni rajhisi kabisa kwa sababu kama nilivyosema, ushahidi wa kilichotokea unajulikana!

No comments:

Post a Comment