Maswali?... Diaby akifikiria mahala pa kupeleka mpira baada ya kuunasa. |
Kula kanzu...! Diaby akifanya vitu vyake |
Abou Diaby ameweka wazi kwamba yeye sio mbadala wa kiungo Alex Song aliyeihama Arsenal msimu huu na kutimkia Barcelona kwa dau la paundi za England milioni 15 (Sh. bilioni 37).
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa ndiye aliyetwaa jukumu alilokuwa nalo Song la kuwa kiungo mkabaji wa Arsenal, lakini amesisitiza kwamba hataki kulinganishwa na Mcameroon huyo kwa vile wao ni wachezaji wawili namna tofauti kabisaaa!
Diaby, ambaye alikuwa ni mchezaji bora wa mechi wa Arsenal wakati wa mechi yao ya Jumapili ya Ligi Kuu ya England waliyoshinda ugenini 2-0 dhidi ya Liverpool, anajiona uchezaji wake kuwa ni wa aina ya Yaya Toure kwavile amekuwa akipanda mbele zaidi kusaidia mashambulizi kadri inavyowezekana na wakati huohuo akitekeleza jukumu la kuzuia.
"Katika timu zetu (Arsenal na Manchester City), Yaya Toure na mimi tuna majukumu yanayofanana," amesema.
"Mimi sio kama Alex Song. Tuna wachezaji wengi wanaoweza kuziba nafasi yake kama Francis Coquelin au Mikel Arteta, ambaye wanapenda kucheza sehemu ya nyuma zaidi. Mimi napenda kusonga mbele -- mimi ni mimi.
"Nina kazi ya kuzuia pia na hivyo ninapaswa kuwa ngangari katika kukaba, na mara tu tunapounasa mpira, nakwenda mbele."
No comments:
Post a Comment