Wednesday, August 15, 2012

ZITTO KABWE AKOMALIA 'CHIMBO' LA VIONGOZI MAFISADI NCHINI USWISI ... NI LILE ALILODAI LINA SH. BILIONI 315 ZILIZOTOKANA NA RUSHWA YA MIKATABA YA UTAFUTAJI MAFUTA NA GESI... ASEMA SERIKALI ISIPOTOA TAMKO, ATAWATAJA WAHUSIKA MMOJA BAADA YA MWINGINE, AKIWEMO KIONGOZI MMOJA WA JUU SANA...!

Mheshimiwa Spika, hii haingii akilini kabisa...! Mhe. Zitto Kabwe akitoa hoja zake bungeni.
Mhe. Ole Sendeka
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Mhe. Zitto Kabwe ameichimba mkwara mzito Serikali kwa kuitaka ichukue hatua dhidi ya wafanyabiashara na viongozi wa serikali waliojilimbikizia zaidi ya Sh. bilioni 315 katika benki mbalimbali za Uswisi kufuatia mapato waliyovuna kupitia rushwa ya mikataba na baadhi ya makampuni yanayojihusisha na utafutaji wa mafuta na gesi nchini.

Mhe. Zitto ambaye pia ni waziri kivuli wa fedha, ameyasema hayo leo wakati akisoma hotuba ya kambi ya upinzani, ambapo bila kuwataja kwa majina, alisema kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua dhidi ya viongozi na wafanyabiashara waliojilimbikizia fedha hizo katika mabenki ya Uswisi na kwamba kinyume chake, kambi yake itawaanika hadharani wahusika wote --  akiwemo kiongozi mmoja aliyedai ni wa juu sana.

Akieleza zaidi, mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema kuwa ukweli kuhusiana na fedha hizo 'chafu' unapatikana kupitia ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Benki Kuu ya Uswisi.

Kufuatia hotuba ya Zitto, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Mhe. Christopher Ole Sendeka alisimama baadaye na kuomba mwongozo wa spika kwa kutumia kanuni namba 68, akitaka kujua ni upande upi utabanwa kati ya serikali na Zitto ili uwataje viongozi wanaohusika na kashfa hiyo moja kwa moja badala ya kuendelea kutoa tuhuma za jumlajumla ambazo zinawachafua hata wasiohusika na pia kuiweka serikali pabaya.

Katika hoja yake, Sendeka alimtaka spika amtake Zitto awataje hao viongozi au Serikali itakiwe kufanya hivyo kwa nia ya kulinda 'image' ya serikali.

Mnadhimu wa kambi ya upinzani na Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Tundu Lissu, alisimama na kusoma vifungu kadhaa vya kanuni za Bunge na kumtaka spika aachane na ombi la Sendeka la kumtaka Zitto abanwe kwavile halikutolewa kwa kuzingatia kanuni.

Naibu Spika, Mhe. Job Ndugai, aliahidi kuipitia vizuri hotuba ya Zitto na baadaye kutoa uamuzi kuhusiana na suala hilo.

No comments:

Post a Comment