Diego Maradona |
GWIJI wa soka wa Argentina, Diego Maradona amefichua dhamira yake ya kutaka kwenda kufundisha China baada ya kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nane ya shughuli za kujitolea, vyombo vya habari vya China vimesema leo.
Maradona (51), kocha aliyeiongoza Argentina katika fainali za Kombe la Dunia 2010, alitimuliwa na klabu ya Falme za Kiarabu ya Al Wasl mwezi uliopita lakini sasa anaonekana kunyemelea kibarua kingine katika mashariki ya mbali.
"Ningependa kufundisha nchini China," Maradona aliuambia mkutano na waandishi wa habari jijini Beijing, gazeti la kila siku nchini humo, China Daily limeripoti leo.
"Napenda kuchangia maendeleo ya soka kwa vijana wa China."
Mmoja kati ya mawakala wa Maradona aliwahi kuitaja pia China mwanzoni mwa mwaka huu, akizungumzia uwezekano wa kuifundisha timu ya taifa ya nchi hiyo, gazeti hilo lilisema.
Wakati wa ziara yake, Maradona, aliyeiongoza timu ya taifa lake kutwaa Kombe la Dunia Mwaka 1986 wakati alipokuwa mchezaji na pia kuchukuliwa kuwa ni miongoni mwa magwiji wa soka wa aina yake waliopata kutokea duniani, atafanya mazungumzo na bosi wa Chama cha Soka cha China, Wei Di.
Maradona, kocha mtata aliyewahi kuwa na matatizo makubwa ya kiafya na pia kupona tatizo la utumiaji wa dawa za kulevya, alitimuliwa katika kibarua cha kuifundisha Argentina baada ya kufungwa na Ujerumani kwa mabao 4-0 katika mechi yao ya robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010.
Hivi karibuni, soka la limeshuhudia ujio wa wachezaji wengi wa kigeni na makocha, akiwamo Sergio Batista, mtu aliyerithi mikoba ya Maradona kuifundisha Argentina na sasa anaifundisha klabu ya Shanghai Shenhua ambako miongoni mwa wachzaji wake ni washambuliaji wa zamani wa Chelsea, Nicolas Anelka na Didier Drogba.
Mahasimu wa jadi wa Shanghai katika Ligi Kuu ya China, klabu ya Guangzhou Evergrande imeamuajiri kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Italia iliyotwaa Kombe la Dunia, Marcello Lippi.
No comments:
Post a Comment